Makala

Vijana wavuruga mkutano wa Bodi ya Usimamizi wa nyumba za bei nafuu

Na SAMMY KIMATU November 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VIJANA katika mtaa wa Makongeni, Nairobi, Novemba 5, 2025 walivuruga mkutano ulioandaliwa na Hazina ya Pensheni ya Waliostaafu katika  Shirika la Reli (KRSRPS) kwa ushirikiano na Bodi ya Nyumba za Bei Nafuu (AHB).

Mkutano huo, uliopangwa kuanza saa kumi alfajiri ulikuwa na lengo la kuelimisha na kushirikisha wakazi kuhusu Mpango wa Uhamishaji wa Wakazi (Resettlement Action Plan – RAP) unaotekelezwa chini ya ajenda ya serikali ya Nyumba za Bei Nafuu.

Hata hivyo, mkutano huo uligeuka kuwa ya vurugu, na kulazimisha maafisa wa usalama kuingilia kati baada ya kundi la watu wenye fujo kujaribu kufunga Barabara ya Jogoo, jambo lililosababisha msongamano wa magari kwa dakika kadhaa.

Akizungumza na Taifa Dijitali, Naibu Kamishna wa Kaunti ya Makadara (DCC), Bw. Philip Koima, alisema mkutano huo ulikuwa umeandaliwa ili kutoa nafasi ya mazungumzo ya wazi kati ya wakazi na wadau wa mradi huo.

“Mkutano huu ulikuwa na lengo la kutoa elimu, kupokea maoni na malalamishi kutoka kwa jamii kuhusu mpango wa uhamishaji, na kuhakikisha kila mtu anaelewa hatua zinazochukuliwa,” alisema Bw Koima.

Mpango wa RAP ni sehemu muhimu ya Mradi wa Nyumba za Bei Nafuu Makongeni, unaolenga kubadilisha nyumba za zamani za Shirika la Reli kuwa majengo ya kisasa yenye ghorofa nyingi.

Bw Koima anasema alipokea taarifa kuwa mwanachama mmoja wa Chama cha Wakazi wa Makongeni (MARA) alihusika kupanga njama ya kuvuruga mkutano huo.

“Baadhi ya viongozi wa MARA waliokerwa na mpango huu wana maslahi ya binafsi. Wamekuwa wakikodisha nyumba za serikali kwa wapangaji wengine kwa bei ya juu kinyume cha sheria,” alisema.

“Mradi mpya unatishia kuvuruga mianya yao ya kupata faida.”

Afisa huyo aliongeza kuwa uchunguzi unaendelea kubaini wahusika, na hatua kali zitachukuliwa mara tu watakapokamatwa.

Wakazi waliokuwa wamehudhuria mkutano huo walionyesha masikitiko kwamba kikao kilichokuwa cha mazungumzo ya amani kiligeuka vurugu.

Wengine walidai walitishwa na kundi la vijana waliokuwa wakipiga kelele, hivyo kushindwa kushiriki katika majadiliano.

Maafisa wa polisi waliokuwa wamepelekwa eneo la tukio walilazimika kuchukua hatua za haraka baada ya waandamanaji kujaribu kufunga Barabara ya Jogoo.

Mradi wa kujenga upya Mtaa wa Makongeni (Makongeni Redevelopment) ni sehemu ya mpango mpana wa serikali wa Nyumba za Bei Nafuu, unaolenga kuwapatia wananchi wa kipato cha chini na cha kati makazi bora na ya heshima.

Hazina ya Pensheni ya Waliostaafu kwenye Shirika la Reli Kenya, ambao unamiliki ardhi na nyumba nyingi eneo hilo, unashirikiana na Bodi ya Nyumba za Bei Nafuu kubadilisha mtaa huo kuwa makazi ya kisasa.

Mradi unajumuisha ujenzi wa majengo marefu ya kisasa, miundombinu bora, shule na vituo vya afya.

Kwa mujibu wa mpango wa uhamishaji, wakazi watapewa makazi ya muda ujenzi ukiendelea, kisha watarudishwa katika nyumba mpya mara ujenzi utakapokamilika.

Utekelezaji wa mpango huu unafanywa kwa awamu.

Mamlaka za eneo hilo zimewataka wakazi kuwa watulivu na kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa mradi huo.