Jamvi La Siasa

Kalonzo asaka nyota ya Raila

Na BENSON MATHEKA November 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, anaonekana kuwa mbioni kusaka nyota ya aliyekuwa Waziri Mkuu Hayati Raila Odinga iangaze azma yake ya urais katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Wachanganuzi wa siasa wanasema hii ilikuwa wazi kupitia ziara yake maalumu ya kumuenzi Raila aliyofanya Alhamisi, Novemba 6, 2025, katika makazi ya Opoda.

Wadadisi wa siasa wanasema kwamba ziara hiyo ilihusisha maombolezo na sherehe za kipekee za urithi wa kisiasa, ishara kwamba Bw Musyoka, sawa na viongozi wengine, anataka kuwarithi wafuasi wa Raila eneo la Nyanza na maeneo mengine.Akizungumza akiwa Opoda, Musyoka alisema “Mtu mwenye haki ya kumuenzi na kuhakikisha jina la Raila Odinga linaishi ni mimi.”

Katika hatua inayothibitisha dhamira yake ya kutaka kuogelea katika bahari ya urithi wa kisiasa wa Raila, alieleza mpango wa wiki nzima wa sherehe za kitaifa za kumuenzi Raila ambazo alisema zitaanza Nairobi na kisha kufanyika katika kila kaunti kwa idhini ya Mama Ida Odinga, mjane wa Raila.

Kulingana na Bw Musyoka, lengo kuu la sherehe hizo ni kutambua mchango mkubwa wa Raila, hasa katika kupigania mageuzi kuhusu ugatuzi.

“Nimemweleza mama Ida kwamba hatujamaliza kumuenzi Raila Odinga. Kwa idhini ya Mama Ida, tutakuwa na sherehe za wiki moja Nairobi kumsherehekea Raila kwa wakati unaofaa, na tutafanya vivyo hivyo katika kila kaunti,” alisema.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki, ziara ya Musyoka ilionekana wazi kuwa njia ya kuimarisha uhusiano kati ya jamii yake ya Wakamba na eneo la Nyanza, ngome ya kisiasa ya Raila, ambapo Kalonzo alisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kitaifa.

“Alianza na kutambua familia ya Raila ambayo ina ushawishi mkubwa wa kisiasa eneo la Nyanza. Matukio katika ziara hiyo yanaonyesha mkakati wa kuwania urithi wa Raila,” alisema Dkt Gichuki.Katika sherehe hiyo, Kalonzo alikabidhi Raila Junior, mwanawe Raila, “vifaa vya mamlaka” ikiwemo upinde na mishale, kiti kidogo, ngao, na mgwisho.

Alieleza kuwa vifaa hivyo ni ishara ya jukumu lake la kulinda urithi wa familia, jamii ya Wajaluo na taifa kwa ujumla.Raila Junior alimpongeza na kuelezea shukrani zake kwa heshima hiyo, akibainisha kuwa jukumu hilo ni zito na linampa nafasi ya kuendelea na urithi wa baba yake.

Aliongeza kuwa baada ya kipindi cha maombolezo, atamtembelea Kalonzo kupata ushauri zaidi kuhusu majukumu yake mapya.“Ni heshima kubwa kwangu, na sitachukulia suala hili kwa wepesi. Naomba kusema asante sana na nitakuja baadaye kwa majadiliano zaidi kuhusu jinsi mimi, Raila Junior, nitakavyoweza kutekeleza jukumu langu kama kiongozi uliyemtawaza,” alisema Raila Junior.

Ida Odinga, mjane wa Raila, alithibitisha kuwa urafiki wa muda mrefu kati ya Kalonzo na Raila hauwezi kufutika.Kalonzo ambaye alimuunga mkono Raila kugombea urais, mara tatu ambapo kati ya hizo ni mara mbili akiwa mgombea mwenza wake, amekuwa akitaja walivyoungana kuandamana kupinga matokeo ya uchaguzi waliodai walipokonywa ushindi kikiwemo kisa cha 2023 ambapo risasi 10 zilifyatuliwa gari la Raila.

Wachambuzi wa siasa wanasema hatua ya Kalonzo ni ya kimkakati kwa kuonyesha mshikamano wa kijamii na kisiasa. Dkt Gichuki anasema ziara ya Kalonzo inaonyesha kwamba anasaka kuendeleza urithi wa Raila Odinga na kuimarisha nafasi yake kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

“Ziara ya Kalonzo Musyoka katika Shamba la Opoda na Kango Ka Jaramogi imeonyesha wazi urafiki wake wa muda mrefu na Raila Odinga, ikithibitisha dhamira yake ya kuhifadhi urithi wa kisiasa na kuutumia kupiga jeki azma yake ya urais kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027,” asema Gichuki.

Hata hivyo, anasema itategemea iwapo mkakati wake utashawishi washirika wa kisiasa wa Raila katika eneo la Nyanza kupitia chama cha ODM.