Makala

Epukeni umbea katika ndoa

Na WINNIE ONYANDO November 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MSHAURI wa masuala ya ndoa na familia, Bi Teresia Watetu, anasema kuwa umbea ni miongoni mwa mambo yanayoharibu ndoa nyingi kimyakimya. 

Kulingana na mshauri huyo, baadhi ya watu wanapenda kusikiza umbea na kusahau kutafuta ukweli.

Wapenzi wengi wamejikuta wakitofautiana, si kwa sababu ya matatizo makubwa, bali kutokana na maneno yaliyosambazwa na watu wanaoitwa marafiki wa karibu.

Anasema kuwa baada ya kutoboa siri zenyu za ndani na marafiki, basi huyo huyo rafiki anaanza kuisambaza kwa wengine.

Hii inaleta aibu na madharau.

Bi Watetu anaeleza kuwa umbea katika ndoa huanza pale ambapo mmoja kati ya wapenzi anaanza kufungua roho na kumwaga siri zao kwa mtu wa nje kama vile rafiki.

“Mara unamueleza jirani, rafiki au ndugu mambo yanayowahusu wewe na mwenzako. Watu hao wanaweza kufasiri vibaya maneno yako na kuyapanua, kisha kuyasambaza kwa wengine.Hii ndio chanzo cha ugomvi katika ndoa au mahusiano ya kimapenzi,” asema.

Kwa mujibu wa mshauri huyo, wanandoa wanaopenda kusikiliza umbea kutoka nje hujipata wakitilia shaka kila jambo. Yaani hata kama yale unayoambiwa ni uongo, wewe utayachukulia kama ukweli.

 “Leo unaambiwa mume wako alionekana na mwanamke fulani, kesho mke wako ameonekana akiongea na mwanaume mwingine. Bila kuthibitisha, unaanza ugomvi. Hapo ndoa inaanza kuyumba,” anaongeza Watetu.

Anasisitiza kuwa msingi wa ndoa imara ni imani na mawasiliano ya wazi. Badala ya kukimbilia kwa watu wa nje, wanandoa wanashauriwa kujadiliana wao wenyewe. “Ukisikia jambo linalomhusu mwenzako, mweleze kwa upole na utulivu. Mnapojifunza kuzungumza kwa uwazi, hakuna nafasi ya umbea kupata mizizi,” anashauri.

Bi Watetu pia anaonya kuwa baadhi ya watu wanaofika kutoa “ushauri” ndio huleta maadhara.

“Sio kila anayekupa sikio anakutakia mema. Wengine wanataka tu kujua siri zako ili wazitumie dhidi yako,” anasema.

Kwa wanandoa, anapendekeza kuwa na mipaka katika urafiki.

“Sio kila jambo la nyumbani ni la watu wa nje. Wakati mwingine, kimya kinaokoa ndoa kuliko mazungumzo yasiyo na maana,” asema Watetu.

Mwishoni, anasisitiza kuwa upendo wa kweli hauwezi kustawi katika mazingira ya umbea na mashaka.

“Wanandoa wakiamua kuaminiana na kuepuka maneno ya watu, watapata amani na furaha ya kweli ndani ya ndoa.”