Uncategorized

Sababu za mahakama kuzima tena usajili wa makurutu wa polisi

Na JOSEPH WANGUI November 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA Kuu jana ilisitisha kwa muda usajili wa makurutu wapya wa polisi kufuatia kesi iliyowasilishwa kupinga uhalali wake.

Kwenye agizo lake, mahakama hiyo ilisema Shirika la Huduma za Polisi (NPS) lingekiuka vipengele kadhaa vya katiba, na kuzidi mamlaka yake, ikiwa lingeruhusiwa kuendelea shughuli hiyo ilivyopangwa.

Eliud Matindi, aliyewasilisha ombi la kusitishwa kwa usajili huo wa makurutu wa polisi, wa cheo cha konstebo, alisema hilo ni jukumu la Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi (NPSC) sio NPS inayosimamiwa na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja.

Kesi hiyo inatokana na matangazo mawili kinzani yaliyotolewa na NPSC na Inspekta Jenerali kuhusu usajili wa jumla ya makurutu 10,000.

Mnamo Septemba 19, 2025, NPSC ilitangaza mipango ya kuendesha usajili huo kati ya Oktoba 3 na Oktoba 9.

Hata hivyo, shughuli hiyo ilisitishwa mnamo Oktoba 2 kufuatia kesi tofauti iliyowasilishwa katika Mahakama ya Uajiri na Mahusiano ya Leba ikisema taratibu hitajika hazikufuatwa.

Wiki kadhaa baadaye, Mahakama ya Leba ilikubaliana na msimamo wa Inspekta Jenerali na ikaharamisha tangazo lililowekwa na tume ya NPSC.

Mnamo Novemba 4, Inspekta Jenerali alichapisha tangazo lingine kuhusu usajili na kuiratibu kufanyika Novemba 17, na hivyo kutohusisha tume ya NPSC.

Inspekta Jenerali alitaja vipengele vya 238, 243, 244 na 245 vya Katiba kutetea msimamo wake kwamba afisi yake ndio yenye mamlaka ya kuwaajiri maafisa wa polisi.

Lakini Bw Matindi, alielekea katika Mahakama Kuu haraka na kudai Inspekta Jenerali ametwaa mamlaka ya kikatiba ya NPSC.

Mlalamishi huyo anashikilia kuwa tume hiyo ya kikatiba ndio yenye mamlaka ya kusajili makurutu wapya wa polisi na kuwapandisha vyeo maafisa wanaouhudumu.

Bw Matindi anashikilia kuwa Inspekta Jenerali amevunja Katiba, kwa sababu hamna sheria inayompa mamlaka kama hayo; isipokuwa iwapo atapewa kibali na tume ya NPSC.

Anasema kuwa kulingana na kipengele cha 246 (3) (a ) cha Katiba, ni NPSC pekee—wala sio afisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi, iliyo na mamlaka ya kuendesha usajili wa makurutu na kuteua maafisa wa polisi.

“Ni msimamo wa mlalamishi kwamba mshtakiwa wa kwanza (Inspekta Jenerali, anayeongoza NPS) hana mamlaka yoyote ya Kikatiba kusajili maafisa wa polisi wa cheo cha konstebo. Katiba imelitwika NPSC jukumu hili,” anasisitiza Bw Matindi.

Anadai kuwa Inspekta Jenerali hakupewa jukumu hilo na NPSC kulingana na Sehemu ya 10 (2) ya Sheria ya Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi.

Kwa hivyo, Bw Matindi anashikilia kuwa shughuli iliyopangwa ya usajili wa makurutu polisi chini ya usimamizi wa Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja ni kinyume cha Katiba na hivyo ni batil