Habari

Kilichofanya Trump kufuta rasmi ziara ya makamu wake nchini

Na STEVE OTIENO November 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAKAMU wa Rais wa Amerika, JD Vance, amefuta rasmi ziara yake iliyopangwa nchini Kenya, mabadiliko yasiyotarajiwa ya kidiplomasia wiki chache tu kabla ya kufika Nairobi.

Kupitia taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Mkuu wa Mawaziri na Wizara ya Masuala ya Kigeni, serikali ya Amerika iliarifu Kenya kwamba ziara ya Makamu wa Rais Vance, iliyopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu, haitafanyika.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba hatua hii imetokana na maagizo ya Rais wa Amerika, Donald Trump, ya kupiga marufuku maafisa wa Amerika kushiriki katika Mkutano wa G20  jijini Johannesburg, Afrika Kusini, ambapo Bw Vance alipangiwa kuongoza ujumbe wa Amerika kabla ya kuzuru Nairobi.

“Serikali ya Jamhuri ya Kenya, kupitia Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigen  imearifiwa na Serikali ya Amerika kuhusu kufutwa kwa ziara iliyopangwa nchini Kenya ya Makamu wa Rais, Mheshimiwa JD Vance, iliyopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Licha ya kufutwa kwa ziara ya hadhi ya juu, Serikali ya Kenya imeonyesha utulivu na uthabiti, ikithibitisha uhusiano wa muda mrefu na Amerika Washington, D.C.

Ziara ya Bw Vance ilitarajiwa kuthibitisha kuongezeka kwa ushirikiano wa Amerika na Afrika Mashariki, wakati ambapo Kenya imejiweka kama nguzo ya kikanda

Makamu wa Rais Vance alitarajiwa kukutana na Rais William Ruto na maafisa wa ngazi za juu wa serikali kwa mazungumzo  kuhusu uwekezaji, usalama, na biashara, hususan chini ya Usimamizi wa Biashara na Uwekezaji wa Kimkakati wa Amerika na Kenya, mfumo uliokusudiwa kuongeza uhusiano wa kibiashara.

Alitarajiwa pia kujadili ushirikiano katika kukabiliana na ugaidi, nishati safi, elimu, na mabadiliko ya kidijitali; sekta ambazo nchi zote mbili zimekuwa zikishirikiana kwa muda mrefu.

Bw Mudavadi alithibitisha imani ya Kenya katika ushirikiano wa muda mrefu na Amerika licha ya mabadiliko hayo ya kidiplomasia.

“Kenya na Amerika zina uhusiano wa kina na wa kihistoria unaohusu heshima ya pande zote, misingi ya kidemokrasia, na maslahi ya pamoja,” alisema Mudavadi, akiendelea kuwa “ingawa mabadiliko ya ratiba mara nyingine hutokea katika kidiplomasia, ushirikiano wetu na Amerika unaendelea kwa nguvu katika sekta zote, kutoka biashara na usalama hadi elimu na teknolojia.”

Aliongeza kuwa Kenya inaendelea kuzingatia kukuza ushirikiano wa kimkakati unaonufaisha pande zote mbili na eneo kwa ujumla.

“Ahadi yetu kwa mazungumzo yenye ufanisi na ushirikiano wa kimataifa haibadiliki. Kenya itaendelea kuwa mshirika wa kuaminika katika kukuza amani, ustawi, na ukuaji wa pamoja,” alieleza.