Walimu wakanusha walikubali kuhamia SHA
WALIMU wameeleza kutoridhishwa kwao na hatua ya serikali ya kuhamisha bima yao ya afya wakilalamikia ukosefu wa ushirikishaji wa umma.
Haya yanajiri saa chache baada ya maafisa wakuu wa vyama vya walimu kusaini makubaliano na serikali kuhamisha bima ya afya ya walimu zaidi ya 400,000 kwa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA),
Uhamisho kutoka bima ya sasa inayotolewa na kundi la kampuni lililoongozwa na Minet Kenya Ltd unatarajiwa kuanza rasmi Desemba 1, 2025.
Hii ilitangazwa wakati viongozi wa vyama vya Kenya (Knut),Kuppet na KUSNET walipokutana na maafisa wa juu wa Tume ya Huduma za Walimu (TSC) na SHA jijini Nairobi.
Hata hivyo, wakuu wa shule za msingi waliohudhuria Kongamano la Mwaka la chama chao (KEPSHA) Mombasa walilalamikia kuhamishwa kwa bima zao kutoka Minet, wakisema hilo limefanyika bila idhini yao.
Walikosoa vyama hivyo kwa kuidhinisha uhamisho bila kushauriana na walimu au kuwaelemisha kuhusu hatua hiyo.
Baadhi yao waliondoka ukumbini mara tu walipopata taarifa kwamba vyama vya walimu vilikubaliana rasmi na TSC kuhusu uhamisho huo.
“Hatutashirikishwa katika mpito huu. Je, jambo muhimu kama hili linaweza kusainiwa nyuma ya mabega yetu?” alisema mwakilishi mmoja aliyeonekana kukasirika, huku wenzake wakiwaka kwa hasira katika ukumbi wa Sheikh Zayed, Mombasa.
Wakuu hao wa shule waliahidi kulalamika katika uchaguzi ujao wa vyama, wakitishia kumfukuza mtu yeyote anayeenda kinyume na matakwa yao. Maafisa wa Knut wanatarajiwa kuzungumza kwenye kongamano Alhamisi huku Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Evaleen Mitei akitarajiwa kufika Jumanne.
“Kuna mapengo mengi ambayo SHA haijashughulikia. Baadhi ya vipimo vya uchunguzi havijafadhiliwa kikamilifu,” alisema Bw Tobias Obuogo, mkuu wa Shule ya Msingi ya Ugina, Homa Bay. Alisema serikali ingepaswa kujaribu mfumo huo awali kabla ya kuanza rasmi.
Sarah Mhonja wa Shule ya Msingi Zimbalo, Vihiga, alisema walimu wengi hawajui kuhusu mpango huo mpya..
Afisa wa KEPSHA kutoka Homa Bay, Bw Moses Kadienge, aliongeza kuwa mchakato huo umeonekana kuwa wa haraka na mgumu kuelewa.
“Tunasikia makubaliano tayari yamesainiwa Nairobi. Wangesubiri wajaribu mpango huo. Kuna haraka sana na uwazi mdogo,” alisema Bw Kadienge, mkuu wa Shule ya Ramba Comprehensive.
Alisema kuwa kukatwa ada za SHA kumepunguza kiasi cha mshahara wa walimu wanaopata mwisho wa mwezi. “SHA imepunguza mshahara wangu. SHA ina changamoto,” alilalamika.
Walimu walisema kuwa Rais William Ruto aliwaahidi bima bora ya afya, si uhamisho wa kulazimishwa.
Walimu hao pia wametaka serikali kutoa uhakika kuwa michango yao itahifadhiwa na haitatumiwa kwa miradi mingine ya afya ya umma, pamoja na ufafanuzi kuhusu jinsi mpito huu utakavyofuatiliwa na kupimwa mafanikio yake.