Habari

Akamatwa kwa kushukiwa kuchoma wajukuu wake kwa chuma moto

Na MERCY KOSKEI November 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAAFISA wa polisi katika Kaunti ya Nakuru wanamzuilia mwanamke mwenye umri wa miaka 60 anayeshukiwa kuwatesa wajukuu wake wawili baada ya kuwalaumu kuiba Sh1,500 zilizokuwa za chama cha akina mama.

Inadaiwa kuwa nyanya huyo aliwakasirikia wavulana hao wenye umri wa miaka 11 na 8, akiwalaumu kwa kuchukua pesa zake, kisha akawachoma kwa kutumia chuma kilichopashwa moto akitaka wawili hao wakiri “wizi” huo.

Baada ya kuwachoma, aliwafungia ndani ya nyumba.

Mwanamke  huyo pia anadaiwa kushirikiana na baba wa kambo wa watoto hao, ambaye ni mwanawe, “kuwafunza adabu,” na kutumia adhabu ya kikatili iliyowaacha wakiwa na majeraha mabaya mikononi na miguuni.

Inaarifiwa kuwa baba wa kambo aliwashikilia watoto hao chini huku nyanya akipasha chuma  moto na kukitumia kuwachoma mikononi na miguuni.

Chifu wa eneo la Mau Summit, Bw Kevin Brown Bett, alisema familia hiyo ilificha tukio hilo kwa wiki moja ili kuepuka kukamatwa, hadi nyanya yao wa upande wa mama, Bi Brenda Chepkemoi, aliporipoti katika kituo cha polisi cha Masaideni, Kaunti Ndogo ya Kuresoi Kaskazini.

Watoto hao walipelekwa hospitalini kwa matibabu huku nyanya yao akikamatwa mara moja. Hata hivyo, baba wa kambo aliyetuhumiwa kushiriki katika tukio hilo anadaiwa kuchoma stakabadhi za polisi na dawa kabla ya kutoroka. Polisi wameanzisha msako kumtafuta.

“Tukio hili lilitokea zaidi ya wiki moja iliyopita, lakini tulilipata Jumanne. Hata kama kweli walikuwa wameiba pesa, hii si njia sahihi ya kuwaadhibu watoto,” alisema Bw Bett.

Aliongeza kuwa wanandoa hao wamekuwa wakigombana mara kwa mara, akitoa wito kwa wazazi kutatua tofauti zao kwa amani badala ya kuwaumiza watoto wasiokuwa na hatia.

Kisa hiki kimezua mjadala mpya kuhusu ongezeko la visa vya unyanyasaji wa watoto ndani ya familia. Mnamo Agosti mwaka huu, msichana wa miaka 9 katika kijiji cha Chepkinoyo, Wadi ya Nyota, alijeruhiwa vibaya na wazazi wake baada ya kudaiwa kuchelewa kurudi nyumbani kutoka kanisani.

Msichana huyo wa darasa la tano alishambuliwa na mama yake Bi Tabitha Wanjiku na baba wa kambo Bw Peter Maina, waliomvua nguo, wakamfunga mikono na kumshambulia kikatili kabla ya kumfungia ndani ya nyumba. Alisaidiwa na majirani na kupelekwa hospitalini, huku mama yake akikamatwa na mwanaume huyo kutoroka.