Habari

Hofu ya maseneta NYS ikigeuzwa kampuni ya kibiashara

Na COLLINS OMULO November 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MPANGO wa serikali ya Rais William Ruto wa kuanzisha tawi la kibiashara ndani ya Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) ili kuliwezesha kujipatia mapato umeibua mjadala mkali katika Seneti.

Serikali inalenga kukusanya angalau Sh4 bilioni kila mwaka kwa kugeuza shirika hilo kuwa kampuni inayotoa huduma za kibiashara. Hata hivyo, maseneta wamehoji uhalisia wa mpango huo, wakisema huenda ni kama serikali inafanya biashara yenyewe.

Maseneta hao pia walitaka serikali kueleza jinsi itahakikisha fedha hizo hazipotei kupitia ufisadi, ikizingatiwa historia ya kashfa zilizowahi kukumba shirika hilo.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Seneti Novemba 13, 2025, Waziri wa Utumishi wa Umma Bw Geoffrey Ruku, alisema serikali iko mbioni kusajili Kampuni ya NYS Enterprise and Services, ambayo itakuwa tawi la kibiashara la shirika hilo.

Alisema kampuni hiyo ya umma itasimamia miradi ya kibiashara ukiwemo ujenzi, kilimo, kusindika mazao, ushonaji, huduma za hoteli na ulinzi, sambamba na ushirikiano na sekta ya kibinafsi katika teknolojia na upatikanaji wa masoko.

Kwa mujibu wa Waziri, kampuni hiyo itamilikiwa kwa asilimia 99 na NYS na asilimia 1 na Wizara ya Fedha, huku usimamizi wake ukiwa tofauti na ule wa NYS.

Bw Ruku alisema serikali hutumia takriban Sh10 bilioni kila mwaka kufadhili mafunzo ya vijana katika NYS, lakini idadi ya wanaojiunga inaongezeka kutoka 18,000 sasa hadi 40,000 Januari 2026, na kufikia 100,000 kufikia mwaka 2027.

“Rasilmali za serikali ni chache, na gharama za mafunzo ni kubwa. Tunahitaji ubunifu ili kupata fedha za kuendeleza mafunzo haya,” alisema.

Hata hivyo, Seneta wa Migori Eddy Oketch alihoji uhalisia wa wazo hilo akisema, “Sielewi kwa nini serikali ifanye biashara na yenyewe. Je, mpango huu ni halisi? Huu ni upuuzi.”

Seneta Mteule Consolata Nabwire naye alitilia shaka iwapo NYS ina mpango endelevu wa kuwezesha shirika hilo kujiendesha.

Lakini Bw Ruku alisema mpango huo ni thabiti na endelevu, kwa kuwa umejengwa katika mfumo wa kampuni yenye usimamizi huru na uwazi wa kifedha.

Seneta wa Mombasa Mohamed Faki alihoji iwapo mpango huo hautaishia kama ule wa mabasi ya NYS wa miaka ya 1980 na 1990 uliofeli vibaya na kuacha serikali na madeni makubwa.

“Kwa nini serikali inageuza NYS kuwa kampuni ya biashara ilhali kazi kama hizo zinaweza kufanywa na watu binafsi?” aliuliza.

Bw Ruku alitaja kifungu cha 7(1)(d) cha Sheria ya NYS ya mwaka 2018, kinachoruhusu shirika hilo kushiriki shughuli za kibiashara ili kusaidia utekelezaji wa majukumu yake ya mafunzo na uwezeshaji wa vijana.

Maseneta Esther Okenyuri na Karen Nyamu walitaka kujua hatua ambazo serikali imeweka kuhakikisha fedha zitakazopatikana hazitapotea kutokana na ufisadi.

Bw Ruku alijibu kwamba serikali imeandaa kanuni maalum za kuhakikisha uwazi, usimamizi bora wa fedha, na kutofautisha kati ya shughuli za mafunzo na biashara.

“Enzi za ufisadi NYS zimepita. Serikali imechukua hatua madhubuti kuhakikisha tunamaliza ufisadi katika shirika hili,” alisisitiza Bw Ruku.