ODM@20: Kaunti ya Mombasa yavuna wageni wakifurika
WAFANYABIASHARA na wawekezaji katika sekta ya utalii wanavuna pakubwa wageni wakimiminika Mombasa, wakiwemo mamia ya wajumbe wa chama cha ODM kutoka kote nchini wanaowasili kwa sherehe za maadhimisho ya miaka 20.
Kando na sherehe hizo za ODM, biashara zimekuwa zikinoga kuanzia Novemba jiji la Mombasa likiwa mwenyeji wa makongamano makubwa ya kitaifa na kikanda, ikiwemo lile la Walimu Wakuu wa Shule za Msingi (KEPSHA).
Miaka iliyopita, ongezeko la wageni lilikuwa likishuhudiwa sana Desemba wakati ambapo msimu mkuu wa utalii hunoga.
Bi Brenda Muli, ambaye anamiliki na kusimamia nyumba kadhaa za kukodisha kwa muda mfupi almaarufu kama Airbnb, anasema sekta hiyo imevuna mwezi huu.
Majumba hayo ya kukodisha yamepita umaarufu mkubwa miongoni mwa watalii wa humu nchini, ikilinganishwa na kukodisha hoteli.
“Nimekuwa nikizungumza na marafiki kujaribu kupata vyumba zaidi kwa ajili ya walimu, ila wengi wamenieleza vimejaa.
Hata wengine walilazimika kuwaomba walimu kutafuta nafasi kwingine,” akasema Bi Muli.
Alieleza kuwa ongezeko hilo la wageni, limemchochea kuboresha nyumba zake ili kuvutia wateja na kuwafanya kurejea tena.
“Ninaomba walimu kadhaa waendeleze likizo yao baada ya kongamano ili tupate hela zaidi. Ninafurahia hata sherehe za ODM, ambazo nina uhakika tayari zishaanza kusisimua uchumi hapa Mombasa. Pwani ni eneo linalopendelewa kwa makongamano na kwa hili tupo tayari,” akasema Bi Muli.
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa Muungano wa Wahudumu wa Hoteli Pwani, Dkt Sam Ikwaye, sekta ya hoteli ni mojawapo tu ya sehemu kubwa ya faida za ongezeko la wageni.
“Si ndege, reli ya SGR, na hata watoaji huduma za usafiri kama vile wanaendesha tuktuk pia wamefaidika,” akasema Dkt Ikwaye.
Dkt Ikwaye, ambaye pia ndiye mwenyekiti wa Baraza la Utalii katika Kaunti ya Mombasa, aliongeza kuwa, eneo limewekeza pakubwa katika utalii na makongamano na kulifanya eneo pendwa kwa hafla kama hizo.
Idadi hiyo kubwa ya watu katika kituo cha reli cha SGR inaonyesha picha kamili ya hali ilivyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli nchini Philip Mainga, alisema kuwa, mipango imewekwa kupata mabogi zaidi, hasa ya Daraja la VIP la treni ya Madaraka Express, kutokana na idadi kubwa wanaotaka tikiti za sehemu hiyo.
Uchunguzi wa haraka wa mtandao wa kukatia tikiti ilionyesha kuwa, treni ya kutoka Nairobi hadi Mombasa, ilikuwa imejaa kwa siku nyingi hadi Februari mwakani.
Katika barabara mbalimbali, waendeshaji tuktuk na bodaboda wanavuna pakubwa, huku wengine wakiongeza bei kuvuna zaidi kutoka kwa wageni.
“Mimi hupata kati ya Sh1,000-1,500 kila siku, ila wiki hii pekee nimekuwa nikienda nyumbani na Sh2,500 au hata zaidi,” akasema Bw Oman Bwanaritzo, mwendesha bodaboda maeneo ya Bombolulu.
Jumanne, zaidi ya wanafunzi 700 kutoka Uganda, waliwasili Mombasa kwa ziara ya kielimu kupitia kwa SGR.