Atwoli aonya wanaosaka kazi nje kwa njia za mkato
KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli, amelalamikia idadi ya Wakenya ambao wanaondoka nchini kusaka ajira ngámbo kisha kukwama huko na kuishia kulaumu serikali.
Kwa mujibu wa Bw Atwoli baadhi hutumia hata njia za mkato kisha kujipata hawana namna na kuanza kulilia serikali wakikamatwa.
Kupitia taarifa, Bw Atwoli aliwataka Wakenya wahakikishe kuwa wanafahamisha ubalozi wa Kenya katika taifa lolote lile wanakosaka ajira.
Hii pia itawaokoa dhidi ya kuandamwa na maajenti wakora ambao huwaahidi mapato mazuri katika nchi hizo kisha wao huishia kuteswa.
“Kenya inaendelea kujiweka kama taifa ambalo linatoa raia wake kufanya kazi katika mataifa ya nje. Hata hivyo, ni vyema iwapo kutakuwa na rekodi yao na pia watambuliwa kupitia asasi zilizopo za serikali.“Hii itahakikisha wanasaidiwa iwapo kuna tatizo ambalo litatokea badala ya kuachwa wakihangaika na maajenti wenye tamaa ya hela,” akasema Bw Atwoli.
Wakati huo huo, Bw Atwoli amewalaumu wanaharakati nchini kupeleka uanaharakati Uganda na Tanzania kisha kukiuka kanuni za kimataifa.
“Nashangaa kuwa baadhi ya Wakenya sasa wanalaumu serikali hasa Wizara ya Masuala ya Nje wakikamatwa mataifa wanakopeleka uanaharakati wao. Hii ni licha ya kwamba wakienda mataifa hayo huwa hawafuati utaratibu unaohitajika kwa sababu wanajua wana hila,” akasema Bw Atwoli.
Kiongozi huyo wa wafanyakazi alisema kuwa kwa zaidi ya miezi sita iliyopita, Cotu imekuwa ikipokea malalamishi ya Wakenya wanaofanya kazi nje kuhusu wanaharakati Wakenya wanaovuruga udhabiti wa nchi nyinginezo.
Alionya kuwa kwa kuvuruga udhabiti wa taifa jingine, raia hao Wakenya wanajiweka katika hatari ya kushtakiwa na kuhukumiwa kulingana na sheria za nchi hizo.
Pia uanaharakati huo hupaka tope serikali na kuiharibia sifa pamoja na kuwachongea Wakenya wanaofanya kazi katika nchi hizo.
“Wanaoenda nje wasiwachochee Wakenya au kutaka wahurumiwe kwa sababu hakuna aliyefahamu sababu zao za kuondoka Kenya na kupeleka uanaharakati wao katika nchi hizo,” akasema Bw Atwoli.
Kiongozi huyo ambaye pia ni Rais wa Muungano wa Wafanyakazi Afrika (OATUU), alikariri kuwa jinsi ambavyo Kenya huwa haivumilii wanaharakati wa nje kuja kuingilia masuala yake ya ndani ndivyo wanaharakati wa hapa nchini wanafaa wakome kuenda mataifa mengine na kuvuruga amani yao.
“Wafanyakazi wote wanastahili kufuata sheria za Kenya kila mahali walipo ndipo hata maslahi yao yatalindwa. Kama Cotu tutaendelea kulinda hadhi ya mfanyakazi Mkenya kila mahali yupo,” akasema Bw Atwoli.