Mchakato wa kujaza nafasi ya Boinnet waanza
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta Jumanne aliwapendekeza watu sita kuwa wanachama wa Tume ya Huduma za Polisi (NPSC) ambayo itapiga msasa atakayechukua nafasi ya Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet anayestaafu mwezi ujao.
Kwenye orodha iliyowasilishwa bungeni, Bw Eliud Kinuthia alipendekezwa kuwa mwenyekiti wa tume hiyo huku wanachama wakiwa ni; Liliam Kiamba, Eusibuta Laibuta, Naftali Kipchirchir Rono, Alice Atieno Otwala na John Ole Mayaki.
Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi aliiamuru Kamati ya Bunge kuhusu Usalama kuwapiga msasa watu hao kisha iwasilishe ripoti yake bungeni mnamo Machi 6, 2019.
“Nawasilisha orodha ya watu hawa waliopendekezwa na Rais kwa kamati kuhusu Usalama iliwa wapigwe msasa kwa muda wa siku 21. Kamati hiyo inapasa kuratibu siku ambayo shughuli hiyo itaendeshwa na iwafahamu watu hao kwa wakati,” akasema Bw Muturi.
Watu hao sita ni miongoni mwa wale ambao walipigwa msasa na kamati teule kwa kipindi cha wiki moja hadi February 1.
Kupendekezwa kwa majina ya makamishna hao wapya wa NPSC kunafuatia kuondoka afisini kwa makamishna wa zamani walioongozwa na Johnston Kavuludi waliohudumu kwa kipindi cha miaka sita.
Wanachama wengine wa tume hiyo ambayo hujishughulisha na masuala yanayohusiana na masilahi ya maafisa wa polisi ni Bw Boinnet, naibu Inspekta Jenerali anayesimamia Polisi wa kawaida Njoroge Mbugua na mwenzake anayesimamia Polisi wa Utawala Noor Gabow.