Samia amteua Nchemba kama waziri mkuu akiingia mahali pa Majaliwa
RAIS Samia Suluhu Hassan jana alimteua aliyekuwa Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo akiingia mahali pa Kassim Majaliwa.
Alichukua hatua hiyo baada ya uchaguzi wa mwezi uliopita ambao uligubikwa na fujo na maandamano.
Bunge lilitarajiwa kuidhinisha uteuzi wa Nchemba hapo jana ikizingatiwa Samia alitangazwa mshindi kwa idadi ya juu ya kura katika uchaguzi huo wa Oktoba 29.
Wapinzani wanadai uchaguzi huo haukuwa na uwazi ndiposa kulikuwa na maandamano kuhusu kufungiwa nje kwa wapinzani wake.
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu kwenye Umoja wa Mataifa (UN) lilisema mamia ya watu waliuawa kwenye maandamana huku upinzani na baadhi ya wanaharakati wakiweka idadi hiyo kuwa zaidi ya watu 1,000.
Serikali hata hivyo imekuwa ikisema kuwa takwimu hizo zilitiwa chumvi japo haijatoa idadi hali ya walioaga dunia.
Samia, amekuwa afisini tangu 2021 na amekuwa akipuuza malalamishi kuhusu rekodi yake ya kuzingatia haki.
Alitetea uchaguzi na ushindi wake kama uliokuwa wa haki na uliostahili.