Habari

Tunatumia chaguzi ndogo kupima utendakazi wetu kura ya 2027

Na JOSEPH WANGUI November 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetaja chaguzi ndogo zijazo Novemba 27 kama mtihani mkubwa kwa uadilifu wake huku ikijitokeza kuwahakikishia Wakenya mchakato wa uchaguzi ulio wa haki na amani.

Haya yamejiri huku vyombo vya usalama na tume ya uchaguzi nchini vikitoa onyo kali kwa wagombea wanaokiuka sheria za kampeni na kutahadharisha kuwa wawaniaji na vyama vya kisiasa watakaopatikana na hatia huenda wakang’olewa kutoka kinyang’anyiro hicho.

Akizungumza Novemba 13, 2025 katika kikao cha kuhutubia vyombo vya habari pamoja na vikosi vya usalama, Mwenyekiti wa IEBC, Erastus Ethekon, alisisitiza kuwa uzingatiaji sheria za uchaguzi sio suala la kujadiliwa, wakitaja chaguzi zijazo kama mtihani muhimu kwa uadilifu wa tume ya uchaguzi.

Bw Ethekon na timu yake walitwaa afisi Julai 2025 na chaguzi ndogo zijazo ni jaribio lao la kwanza kubwa kusimamia.

“Huu ni mtihani kwetu,” alikiri Bw Ethekon katika jumba la Anniversary Towers, akiandamana na Mkuu wa Polisi, Douglas Kanja na Bosi wa Tume ya Uwiano, Samuel Kobia.

“Tulipoteuliwa, sisi (makamishna wa IEBC) tulikula kiapo cha afisi, na tunafanya kila liwekanalo kuhakikisha chaguzi zinafanikiwa.”

Alisema tume imefanya maandalizi ya kina, ikiwemo kuwapa mafunzo maafisa wa uchaguzi, kusambaza vifaa na kutekeleza ratiba madhubuti za kampeni ili kuzuia machafuko.

Matamshi yake yalijiri wakati ambapo wasiwasi umetanda kuhusu ghasia za uchaguzi, hasa katika eneobunge la Kasipul ambapo mapigano kati ya wafuasi mahasimu yaliripotiwa.

IEBC imeagiza wagombea husika kujiwasilisha kwake na kuonya ukiukaji wa kanuni za uchaguzi na nidhamu utasababisha kubanduliwa.

“Tunakemea ghasia za kikatili zilizofanyika Kasipul,’ alisema Bw Ethekon.

“Kanuni ya kinidhamu ni thabiti – siyo pendekezo – na tutawachukulia hatua wanaokwenda kinyume.”

“Wagombea wote na vyama vyote vya kisiasa wako huru kuendesha kampeni katika maeneobunge yao mt