Habari

ODM@20: Orengo, Winnie wasema ODM haiendi kwa Ruto

Na WACHIRA MWANGI November 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

VIONGOZI wakuu wa ODM wamesema chama hicho hakipo sokoni huku wakihimiza umoja, ujasiri na uaminifu jinsi  ilivyokuwa enzi za marehemu Raila Odinga .

Akihutubia hadhira ya vijana jijini Mombasa kwenye maadhimisho ya ODM@20 katika ukumbi wa Swahilipot, Gavana wa Siaya James Orengo alipinga madai kuwa kuna mgawanyiko na shinikizo za ili wamuunge mkono Rais William Ruto mnamo 2027.

Bw Orengo alisisitiza kuwa ODM itasalia  huru tena kwenye upinzani wala hakitayumbishwa na ari ya baadhi ya wanasiasa kuiingiza serikalini.

“Tunasikia watu wakiongea kuhusu makubaliano na Serikali Jumuishi. Isisahaulike kuwa chama kikuu cha upinzani, katika bunge la kitaifa na lile la Seneti, ni ODM. Hatutanyamaza,” alisema Bw Orengo.

Bi Winnie Odinga, ambaye alithibitisha uaminifu wa familia kwa chama baada ya kifo cha babake, alipuuzilia mbali madai ya misimamo tofauti ndani ya ODM.

“Nimesikia watu wakisema kuna mgawanyiko ndani ya chama, wasahau hilo. Wakati wa msiba, watu huchanganyikiwa. ODM ilijengwa kwa mapambano na katika kipindi cha  miaka 20 watu wamelia na kupigania chama,” akasema.

“Wapo wanaotembea nasi mchana lakini usiku wanajadili chama katika mazungumzo ya faraghani. Hilo halitabadilisha lolote kwa sababu ODM haiwezi kumezwa. Hiki ni chama cha watu, hakikuzaliwa kwa sira na  hatima yake haiwezi kuamuliwa kisirisiri.” akaongeza Bi Winnie.

Bw Orengo aliirejelea historia ya vyama vya ukombozi barani Afrika, akionya kuwa chama chochote kinachopuuza nguvu ya vijana mwisho wake hupoteza mwelekeo.

Seneta huyo alikerwa na msukumo kuwa ODM inastahili kumuunga Rais Ruto akisema ,”Ruto anahitaji ODM; si ODM inamhitaji Ruto. Nasema bila woga.”

Aliwafokea wanaodai ODM haina uwezo wa kutoa mgombea urais akisema,“Wanaosema hatuwezi kutoa mgombea urais wanaonyesha upumbavu.”

Alikosoa wazo la mkataba wa kisiasa na serikali: “Mkataba wa MOU hauwezi kutekelezwa chini ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa.”