Joho njia panda kisiasa vita vya ODM vikichacha
MISUKOSUKO katika Chama cha ODM imeweka hatarini azma ya Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini, Bw Hassan Joho, ambaye amekuwa akimezea mate wadhifa mkubwa zaidi serikalini baada ya uchaguzi ujao.
Kwa muda mrefu tangu Rais William Ruto na aliyekuwa kinara wa ODM Raila Odinga walipoweka makubaliano ya kushirikiana, Bw Joho na wandani wake Pwani wamekuwa wakisisitiza kwamba anastahili kupewa wadhifa mkubwa serikalini ushirikiano huo ukidumu baada ya uchaguzi ujao, huku akipanga kuwania urais katika chaguzi za baadaye.
Wakati wa mkutano wa hadhara Jumamosi, Novemba 15, 2025 jijini Mombasa kuadhimisha miaka 20 tangu ODM ianzishwe, Bw Joho alionyesha wazi anavyokerwa na baadhi ya viongozi wanaopinga ushirikiano wa chama hicho na serikali ya Dkt Ruto.
“Nakilinda chama changu kwa damu na kwa juhudi zangu zote. ODM imefika ilipo kwa sababu baadhi yetu tulijitoa kwa udi na uvumba. Mara pekee niliyowahi kusumbuliwa na polisi na kukwepa risasi ni kwa sababu ya chama na kwa kumuunga mkono Bw Odinga.
“Baadhi yetu tuliingia ODM tukiamini kwamba sisi Wapwani pia siku moja tungekuwa na ndoto ya kuwa Rais wa Kenya. Msifikiri mtatutoa kafara. Hatuwezi kutumiwa kama sadaka. Sijawahi kufuata chama kingine zaidi ya ODM. Mkinifukuza, nitawafukuza. Kikiharibika, kiharibike,” alifoka Bw Joho.
Hotuba hiyo ilishabikiwa na wabunge wa Pwani ambao walisisitiza kwamba Bw Joho ndiye bado nguzo ya kisiasa eneo hilo.
Jumapili, wakati wa mkutano wa maombi Kaunti ya Kilifi uliokamilisha sherehe za kuadhimisha miaka 20 ya ODM, wanasiasa wa Pwani waliendeleza kauli hizo.
Mbunge Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Mombasa, Bi Zamzam Mohamed, alisema misimamo mikali inayoendelezwa na baadhi ya wanachama akiwemo Katibu Mkuu, Bw Edwin Sifuna, kuhusu ushirikiano na serikali ya Kenya Kwanza, inamkosea heshima Bw Joho.
“Watu wanaozungumza sana wakitaka kutugawanyisha, tunawaambia sisi Wapwani tunaangalia kwa makini. Hatuwezi kusukumwa nje ya ODM, lazima waheshimu Hassan Joho, wajue alipigania chama,” akasema.
Mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko, alisimulia jinsi Bw Joho alivyowahi kutishiwa maisha alipokuwa gavana wa Mombasa kwa sababu ya misimamo yake ya kutetea chama na Bw Odinga.
Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Mung’aro, aliwakosoa viongozi wanaosisitiza kwamba ODM haiwezi kuungana na wengine.
Kulingana naye, Raila alionyesha nia na umuhimu wa ushirikiano tangu alipoanza kuungana na viongozi katika chaguzi zilizopita au baada ya chaguzi na hilo halifai kufutiliwa mbali.
“Tuache kusema hatuwezi kuungana na wengine. Hatuwezi kuunda serikali bila kuungana na wengine. Tushirikiane kwanza kama ODM na tuache kutoa masharti, halafu tushikane na wengine ambao wanataka kuunda serikali na sisi. Tunahitajiana sote, hakuna walio bora kuliko wengine katika hiki chama,” akasema Bw Mung’aro.
Mwenyekiti wa chama, Bi Gladys Wanga, alisema tofauti zilizoibuka chamani zitatatuliwa kwani wanachama wameonyesha nia ya kutaka kusalia ndani ya chama licha ya malumbano. Gavana wa Mombasa, aliye pia mmoja wa manaibu viongozi wa ODM, Bw Abdulswamad Nassir, alisema uongozi mpya wa chama una jukumu kubwa la kuleta umoja katika chama.