Habari

Ashtakiwa kwa kuitisha hongo ya Sh5M

Na RICHARD MUNGUTI November 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWENYEKITI wa mamlaka ya kupambana na uuzaji wa bidhaa bandia (ACA) ameshtakiwa kwa kudai hongo ya Sh5milioni kutoka kwa muuzaji wa vipuri vya magari.

Josphat Gichunge Kabeabea aliyekabiliwa na mashtaka matano alishtakiwa Jumatatu (Novemba 17,2025) mbele ya hakimu mkazi Celesa Okore.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga alieleza mahakama, Kabeabea alidai hongo hiyo ya Sh5milioni kutoka kwa mwekezaji Du Zhiseng anayeuza vipuri vya magari.

Kinara huyo wa ACA alidaiwa alimtaka Zhiseng atoboke mlungula huo ili asimtie nguvuni na kumfungulia kesi ya kuuza vipuri feki vya magari.

Mahakama iielezwa Zhiseng alikataa kuachilia hongo ya Sh5milioni ndipo Kabeabea akaanza kuipunguza kwa Sh4milioni hadi Sh1milioni.

Zhiseng pia alikataa kutoa mlungula huo wa Sh1milioni.

Kabeabea, hakimu alielezwa, aliteremka kutoka Sh1,000,000 hadi Sh300,000 ambazo mlalamishi alikataa kuzitoa ndipo kinara huyo wa ACA akapunguza hadi Sh144,500 ambazo alitumiwa kupitia wa Ntorui Erustus Kaibi.

Kabeabea alishtakiwa kwamba mnamo Novemba 11,2025 mahala pasipojulikana humu nchini alimtaka Zhiseng amhonge kwa Sh5milioni ndipo akwepe kukamatwa na kushtakiwa kwa kuuza vipuri feki vya magari.

Korti iliezwa na DPP kwamba mshtakiwa alidai pesa hizo mnamo Novemba 11,2025 kwa lengo la kumwokoa asifunguliwe mashtaka ya kuuza vipuri feki katika kampuni yake iliyoko jijini Nairobi.

Mshtakiwa alikana mashtaka hayo ya kupokea hongo na kupatikana na pesa ilizopata kwa njia ya uhalifu.

Kabeabea alikamatwa na maafisa wa tume ya kupambana na ufisadi EACC Jumatatu asubuhi na kufululizwa moja kwa moja hadi kortini baada ya alama zake za vidole kuchukuliwa.

Mshtakiwa aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana huku akiahidi kutii maagizo atakayo pewa na mahakama.

Upande wa mashtaka haukupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Akitoa uamuzi hakimu alisema dhamana ni haki ya kila mshukiwa.

“Dhamana ni haki ya kila mshukiwa anayopasa kupewa na mahakama. Haki hii inaweza tu kutwaliwa endapo mshtakiwa ni tisho kwa utekelezaji haki,atavuruga mashahidi ama kutoroka akiachiliwa,”hakimu Celesa Okore alisema akiamua ombi la dhamana.

Bi Okore alimwachilia kwa dhamana ya Sh1milioni pesa tasilimu.

Hakimu aliamuru kesi itajwe baada ya wiki mbili itengewe siku ya kusikizwa.

Pia Bi Okore aliamuru upande wa mashtaka umpatie mshtakiwa nakala za mashahidi aanze kuandaa ushahidi atakaowasilisha kortini akijitetea.

Kabeabea alipelekwa gerezani kuzuiliwa akitafuta pesa za kulipia dhamana hiyo ya Sh1milioni pesa tasilimu.