Michezo

Wanariadha waliopigwa marufuku kwa kusisimua misuli wakiri kuwa na mawazo ya kujitia kitanzi – Utafiti

Na GEOFFREY ANENE November 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

UTAFITI mpya umebaini athari kali za kisaikolojia kwa wakimbiaji wa Kenya waliopigwa marufuku kwa madai ya kutumia dawa za kusisimua misuli.

Utafiti huo uliotolewa Novemba 1 na Byron O. Juma na Jules Woolf nchini Amerika ulihusu mahojiano na wanariadha 10 waliofungiwa na maafisa watatu wa kukabiliana na matumizi ya pufya.

Kenya inayoorodheshwa kama taifa “lenye hatari kubwa,” ina zaidi ya wanariadha 100 wa mbio za kati na ndefu wakiwemo mastaa Lawence Cherono na Ruth Chepngetich wanaotumikia adhabu za matumizi ya pufya.

Wanariadha, ambao majina yao yalibanwa, walieleza mshtuko, kuchanganyikiwa na msongo mkubwa baada ya kuarifiwa wamepatikana na vitu vilivyopigwa marufuku mwilini, jambo lililoonyesha pengo kubwa la uelewa kuhusu udhibiti wa matumizi ya dawa za kusisimua, hata miongoni mwa wanariadha wa kimataifa.

Wengi walihisi aibu na waliogopa kutajwa kama walaghai. Baadhi walijitenga kwa miezi, na kuongeza mfadhaiko, huku wengine wakizamia pombe. Wasiwasi kuhusu kupoteza kipato na kutoweza kusaidia familia ulienea, na baadhi walipata matatizo ya kiafya kama vidonda vya tumbo.

Unyanyapaa kuhusu afya ya akili nchini Kenya uliwaacha wengi bila msaada. Wakati wanariadha saba kati ya 10 waliripoti kuwa na mawazo ya kujitia kitanzi, mmoja alijaribu kujiua kabla ya kuokolewa na majirani na kulazwa katika kituo cha afya ya akili. Wengi walikumbana na kejeli za jamii, kuharibiwa sifa na migogoro ya kifamilia, ikiwemo kutengana na talaka. Watoto wao pia walishutumiwa.

Katika utafiti huo, wanariadha walisema Shirikisho la Riadha Kenya liliwatelekeza baada ya kupigwa marufuku, bila kutoa msaada wa kisaikolojia. Watafiti wanashauri kuwepo sera za huduma za afya ya akili, msaada kwa familia, na mipango ya kuwawezesha wanariadha kurejea au kuanza upya maisha bila madhara makubwa ya baadaye.