Habari

Mapenzi ya mtandao ni sumu, DCI yaonya

Na ERIC MATARA November 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

IDARA ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imewaonya Wakenya na wageni dhidi ya kutafuta mapenzi mtandaoni.

Hii inatokana na ongezeko la visa vya utapeli hasa kwenye majukwaa ya kusaka wachumba ambapo watapeli wanatumia nafasi hizo kuwapora wahusika pesa na mali zao.

Wiki chache zilizopita, raia wa Uingereza aliyekuwa akitembelea Mombasa alipoteza zaidi ya Sh800,000 baada ya kudanganywa na walaghai aliokutana nao kupitia mtandao wa kuchumbiana.

Siku chache baadaye, Novemba 11, 2025, maafisa wa DCI waliwakamata washukiwa wawili wa genge la wahalifu wanaoendesha ulaghai wa mapenzi mtandaoni eneo la Nyali, Mombasa.

DCI ilisema kundi hilo huwavutia wageni kupitia mahusiano ya kimapenzi mtandaoni kisha kuwanasa katika mtego wa uporaji.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa DCI, Mohamed Amin, mwanamke mmoja wa Mombasa alianza uhusiano wa kimapenzi mtandaoni na mtu kwa miezi kadhaa kabla ya kumvuta nyumbani kwake.

Lakini alipowasili kwenye nyumba hiyo, mtego ulikuwa tayari umeandaliwa.

Dakika chache baada ya kumkaribisha, wanaume wawili waliokuwa washirika wa mwanamke huyo walivamia nyumba hiyo.

Mmoja alijifanya kuwa mumewe aliyekuwa na hasira, huku mwenzake akijifanya afisa wa polisi aliyekuwa na kitambulisho feki na kumtishia mzungu huyo kwa madai ya “kuvunja ndoa.” Mwathiriwa alilazimishwa kutuma Sh800,000 kwa nambari za simu alizopatiwa.

Baada ya hapo, alifukuzwa na genge hilo lililotoweka usiku.

DCI ilisema uchunguzi wa kiteknolojia uliwawezesha maafisa kunasa mwanamke huyo na mshukiwa mwingine, huku msako wa kutafuta wa tatu ukiendelea.

Uchunguzi wa DCI umebaini kuwa kundi hilo ni sehemu ya mtandao wa wizi unaoandaa uhusiano feki mtandaoni kabla ya kuwaalika waathiriwa katika nyumba za kifahari au Airbnb za maeneo ya watalii kama Nyali, na kuwateka kwa vitisho.

“Uchunguzi umeonyesha kuwa washukiwa ni sehemu ya mtandao unaowavizia wageni mtandaoni kisha kutekeleza uhalifu unaopangwa katika makazi ya faragha,” alisema Amin.

Katika kisa kingine Nakuru wiki mbili zilizopita, mwanamume alipoteza Sh400,000 baada ya kudanganywa na mwanamke aliyekutana naye kwenye tovuti ya kusaka wachumba. Alitekwa katika nyumba ya kifahari Milimani na kuporwa.

Mwezi uliopita, mwanamke jijini Nairobi aliiba Sh300,000 kutoka kwa mfanyabiashara baada ya kukutana naye kupitia mitandao ya kijamii na kupanga miadi katika klabu moja mtaani  Lavington. Usiku, mwanamke huyo alitoa fedha kutoka kwa simu ya mwathiriwa wake hadi kwa akaunti yake.

Kulingana na DCI, Visa hivi, si vya kipekee. Ni sehemu ya ongezeko la uhalifu wa mtandaoni kwa kutumia udhaifu wa hisia kuwahadaa watu.

Katika onyo lake la karibuni, DCI ilisema kumekuwa na ongezeko la visa vya wizi wa kimabavu na ulaghai wa kifedha vinavyoanzia kwenye mahusiano ya mtandaoni.

“Tunatoa tahadhari kwa wananchi kuhusu ongezeko la visa vya watu kudanganywa kupitia majukwaa ya uchumba mtandaoni na kuvutwa hadi maeneo hatari,” ilisema DCI.

Kwa mujibu wa idara hiyo, wahalifu hutumia ujanja wa kisaikolojia kujenga uaminifu bandia kabla ya kutaka kukutana ana kwa ana wanayelenga.

“Wahalifu hawa wana uwezo mkubwa wa kutumia hisia za watu kupata taarifa binafsi na kifedha,” iliongeza DCI.

DCI inataka watu kuwa waangalifu wanapowasiliana na watu mtandaoni hasa wakati huu wa msimu wa sherehe.

Usisambaze taarifa nyeti, ikiwemo nambari za kitambulisho, taarifa za benki, mahali unapoishi, au mipango ya safari.

Idara hiyo pia imesisitiza kuwa mikutano ya ana kwa ana ifanyike maeneo ya wazi na yenye ulinzi kama vile mikahawa, vituo vya ununuzi au hoteli zilizo na watu.

“Kabla ya kukutana na mtu, mjulishe rafiki au mwanafamilia unayemuamini, ukiweka wazi utakapokuwa na saa ya mkutano,” DCI ikaongezea.

Idara hiyo imewahimiza waathiriwa kuripoti visa vya kutiliwa shaka mara moja.

“Ikiwa utajikuta katika hali ya hatari, kata mawasiliano mara moja na utafute msaada. Ripoti kwa kituo cha polisi au ofisi ya DCI,” ilisema.