Habari

Wasiwasi uchaguzi wa viongozi wa kitaifa utavunja ODM

Na MOSES NYAMORI November 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

BAADHI ya wanachama wa ODM sasa wanataka chama hicho kiitishe Mkutano wa Baraza la Kitaifa la Wajumbe (NDC) ili kuchagua viongozi wa kitaifa.

Haya yanajiri huku wanachama wakionekana kutofautiana hasa kuhusu suala la kuunga mkono serikali jumuishi.

Kambi mbili zinazotofautiana zimeibuka, huku moja ikidai kiongozi mpya wa chama Dkt Oburu Oginga yupo ofisini kinyume cha sheria bila idhini ya baraza kuu la chama.

Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, na Godfrey Osotsi (Seneta wa Vihiga), Abdulswamad Nassir (Gavana wa Mombasa) na Simba Arati (Gavana wa Kisii) pia hawajaidhinishwa na NDC.

Hata hivyo, viongozi hao walithibitishwa na Baraza la Kitaifa la Usimamizi la Chama (NGC) Oktoba 13 2025.

Wale wanaotaka mkutano wa NDC wanataja Kifungu cha 6.2 cha katiba ya chama kuhusu uchaguzi wa viongozi wa kitaifa.

Kifungu hicho kinasema kuwa “Endapo Kiongozi wa Chama atashindwa kutekeleza majukumu yake kwa sababu ya udhaifu wa mwili au akili, kifo, kujiuzulu au anapoacha kuwa mwanachama, Kikao maalum kitaitishwa ili kumchagua Kiongozi mpya wa Chama.”

Baadhi ya viongozi wa ODM ambao wamepinga hadharani uongozi wa Dkt Oburu ni pamoja na Winnie Odinga, binti wa marehemu kiongozi wa chama Raila Odinga, Mbunge wa Saboti Caleb Amisi na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino.

Kutokuwepo kwa Bw Odinga, kunaonekana tishio kubwa kwa umoja wa chama kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Kundi linalounga mkono Serikali Jumuishi linasema, ni sehemu ya mpango mpana wa kusukuma chama ndani ya uchaguzi wenye mgawanyiko, na lengo kuu ni kufanya chama kuingia uchaguzi wa 2027 kikiwa kimevunjika.