Habari

Kalonzo, Gachagua chonjo kuhusu 2027, wafika kortini

Na JOSEPH WANGUI November 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MUUNGANO wa viongozi wa upinzani unaoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, umewasilisha kesi mahakamani wakitaka kubadili kabisa namna matokeo ya uchaguzi wa urais yanavyohesabiwa, kutumwa na kutangazwa.

Katika kesi yao iliyowasilishwa katika Kitengo cha Katiba na Haki za Binadamu cha Mahakama Kuu jijini Nairobi, wanataka maagizo manne makuu, ikiwemo kuilazimisha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutangaza rasmi vituo vya kupigia kura angalau miezi sita kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Pili, wanataka matokeo ya mwisho ya kura za urais yaamuliwe katika ngazi ya eneo bunge.

Tatu, wanataka mahakama iamuru ujumuishaji wa kura kufanyika moja kwa moja katika kituo cha kupigia kura.Agizo lingine kuu wanaloomba ni kutangazwa kuwa sheria ya sasa ya IEBC na mwenyekiti wake kukusanya na kutangaza matokeo ya urais katika kituo cha kitaifa cha kujumuisha kura ni kinyume cha Katiba na haitii sheria.

Kulingana na ombi hilo, IEBC inadaiwa kukiuka Katiba kwa kushughulikia matokeo ya urais katika kituo cha kitaifa badala ya yanavyotumwa kutoka kwa maafisa wa maeneo bunge.

“Kituo cha kitaifa kinapaswa tu kutangaza matokeo yanayopokewa kutoka maeneo bunge, si kuyabadilisha au kuyakataa,” akasema wakili wao Gitobu Imanyara.

Mbali na Bw Gachagua na Bw Musyoka, wengine ni pamoja na Fred Matiang’i (Jubilee), Justin Muturi (Democratic Party), Eugene Wamalwa (DAP-K), Mithika Linturi (DCP), na Martha Karua wa People’s Liberation Party (PLP).Wanadai kuwa kushindwa kwa IEBC kutangaza vituo vya kupigia kura mapema, ikifanya hivyo wakati mwingine wiki chache kabla ya uchaguzi, kunahatarisha uwazi wa uchaguzi.

Muungano wa upinzani unasisitiza kuwa mfumo wa sasa wa “ukaguzi wa pili” wa matokeo ya urais katika kituo cha kitaifa umekuwa chanzo cha mkanganyiko, kwa kuwa unafungua mianya ya udanganyifu na kupunguza imani ya umma.

Wanataja chaguzi za 2013, 2017 na 2022 kama ushahidi wa migogoro inayoendelea kutokana na mfumo huo.

Wanasisitiza kuwa matokeo ya urais yanayotangazwa na maafisa wa uchaguzi wa maeneo bunge yanapaswa kuwa ya mwisho, sawa na yale ya wabunge na wawakilishi wa wanawake.

Hoja kuu katika ombi hilo ni kuwa mfumo wa sasa unakiuka Ibara ya 138(2) ya Katiba inayosema kuwa uchaguzi wa urais “utafanyika katika kila eneo bunge.”

Kwa hivyo, wanasema jukumu la kitaifa linapaswa kuwa kujumlisha tu matokeo na si kuyachunguza upya.Katika kiapo chake, Bw Musyoka analaumu IEBC kwa kukiuka kanuni za uwazi, uwajibikaji na ushirikishaji wa umma kwa kuchelewesha sajili ya wapiga kura.

Alinukuu pia maoni ya Mahakama ya Juu katika kesi ya urais ya 2022 kuhusu kucheleweshwa kwa sajili ya wapiga kura ambayo ilisababisha wasiwasi mkubwa.

Waombaji wanahofia kuwa bila mageuzi, Kenya itaendelea kukumbwa na migogoro ya uchaguzi, ikiwemo madai ya “vituo hewa” na dosari katika sajili ya wapiga kura.

Wanapendekeza muda maalum wa miezi sita kwa vituo vya kupigia kura kuchapishwa katika gazeti rasmi na miezi mitatu kutangaza sajili ya wapiga kura ili umma uipitie mapema.

Wanataka mahakama iagize kuwa matokeo ya urais katika maeneo bunge ndiyo ya mwisho; kwamba IEBC izuiwe kubadilisha matokeo katika kituo cha taifa; na kwamba ujumuishaji wa kura ufanywe kabla ya kutuma matokeo.

Wanadai hakuna msingi wa kikatiba unaoruhusu uchaguzi wa urais kuwa tofauti na chaguzi nyingine. Kwa mujibu wa Bw Musyoka, “kuunda mfumo tofauti wa kusimamia matokeo ya urais ni ubaguzi usio na msingi wowote wa kikatiba.”

Katika kesi hiyo, IEBC, mwenyekiti wake na Mwanasheria Mkuu wametajwa kama washtakiwa, huku walalamishi wakisema masuala hayo ni ya maslahi ya umma na kesi inalenga kulinda demokrasia ya Kenya.