Ruto ahutubia taifa Wakenya wakilia hali ngumu ya maisha
MWAKA mmoja baada ya Rais William Ruto kuahidi kwamba atamaliza changamoto zinazokabili sekta ya afya, kupunguza gharama ya maisha na kuimarisha uchumi wa nchi, ni ufanisi mdogo ndio umepatikana Wakenya wakiendelea kukumbana na changamoto tele.
Akihutubia taifa kupitia kikao cha pamoja cha Bunge na Seneti mnamo Novemba 21, 2024, Rais Ruto aliahidi kuwa lengo lake lilikuwa kuinua nchi na kusaidia isisambaratike kiuchumi.
“Kupitia Sheria ya Kidijitali ya Afya, tunabadilisha utoaji huduma katika sekta ya afya. Mpango wa Huduma za Afya kwa Wote (UHC) unasalia ajenda yetu kwa sababu inagusia kila familia,” akasema Rais Ruto huku wakati huo akikisia Sh122 bilioni zingetumika katika kuinua sekta ya afya.
Hata hivyo, deni la Sh76 bilioni ambalo Bima ya Afya ya Jamii (SHA) inadaiwa na hospitali na vituo vya afya imesababisha Wakenya waingie mfukoni zaidi na sasa gharama ya afya iko juu.
“Kenya itakuwa na sekta ya afya ambayo ina thamini huduma kwa binadamu, amani na usawa kwa Wakenya kwa mara ya kwanza kwa miaka 60 tangu tupate uhuru,” akasema Rais Ruto wakati huo.
Muungano wa Hospitali za Kibinafsi Mijini na Mashambani (RUPHA) ambao unasimamia zaidi ya hospitali na vituo vya afya 380 unadai serikali Sh15 bilioni kati ya deni hilo la Sh76 bilioni.
Kukosa kulipa madeni ya kimatibabu kumeshuhudia hospitali chini ya RUPHA zikatae kadi za SHA na sasa wanaotaka matibabu wanalazimika kulipa kutoka kwa mfuko wao.
Licha ya changamoto za SHA, takwimu za kiuchumi zinaonyesha kuwa idadi ya hospitali zimepanda kwa asilimia 6.1 hadi 15,984 mnamo 2025.
Idadi ya vitanda hospitalini pia iliongezeka na kupanda kwa asilimia 15.5 hadi 115,786.
Mnamo 2024 Rais Ruto aliambia nchi kuwa hali nzuri ya hali ya hewa iliongeza uzalishaji wa chakula na kusaidia mfumuko wa kiuchumi kutokea asilimia 9.6 mnamo Septemba 2022 hadi asilimia 2.7 mnamo Oktoba 2024, idadi ya juu zaidi ndani ya miaka 17.
Rais alisema kuwa kuimarika kwa uzalishaji wa chakula kumechangia kupunguza bei ya chakula ikiwemo nafaka, mahindi na maharagwe.Kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa kiuchumi 2025, Kenya ilipunguza vyakula vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi kwa asilimia 17.3 mnamo 2024.
SHA“Bei ya chakula na kawi pamoja na udhabiti wa shilingi ya Kenya ndiyo ulisaidia kupunguza mfumuko wa kiuchumi,” utafiti wa kiuchumi ulieleza.Aidha utafiti huo ulionyesha kuwa idadi ya vituo vya masomo ilipanda kwa asilimia 38.3 hadi 129,463 mnamo 2024 baada ya kujumuisha shule za sekondari msingi.
Taasisi za Mafunzo ya Kiufundi na Vyuo Anuwai (TVETS) nazo ziliongezeka kwa asilimia 6.9 hadi 2,756 mnamo 2024 kutokana na kuongezeka kwa vituo vya mafunzo ya kiufundi ambavyo viliidhinishwa.
Idadi ya vyuo vikuu navyo vilipanda hadi 72 mnamo 2024 kutoka 70 mnamo 2023 baada ya Chuo Kikuu cha Tangaza na kile cha Kitaifa cha Utafiti (NIRU) kupewa vyeti na serikali.
Mamlaka ya Kitaifa ya Uajiri (NEA) ambayo ina mamlaka ya kubuni nafasi za ajira kwa Wakenya ambao wamehitimu ndani na nje ya nchi, kwa sasa ina nafasi 560,000 za ajira kote ulimwenguni.Wakenya walioajiriwa sekta ya juakali na nyingine ambazo si za serikali ilipanda kutoka milioni 20 mnamo 2023 hadi milioni 20.8 mnamo 2024.
Hii inaonyesha kuwa nafasi 782,000 za ajira zilibuniwa mnamo 2024 huku serikali ikitoa 78,000 na sekta zisizo rasmi zikibuni nafasi 703,000 za ajira.