Habari

Museveni afichua wanaharakati wa Kenya waliwekwa katika friji

Na KEVIN CHERUIYOT November 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni, amethibitisha kwamba serikali yake iliwakamata wanaharakati wawili wa Kenya, Bob Njagi na Nicholas Oyoo kisha kuwazuilia bila mawasiliano kwa siku 38 baada ya kupokea taarifa za kijasusi zinazowahusisha na kiongozi wa upinzani Robert Bobi Wine Kyagulanyi.

Akizungumza kwa mara ya kwanza kuhusu suala hilo katika kipindi cha redio kilichofanyika katika Ikulu ya Mbale, Rais Museveni alisema Wakenya hao wawili ni “wataalamu wa maandamano” na walikuwa wakishirikiana na kundi la Kyagulanyi kuingiza Uganda katika machafuko.
“Tuna taarifa nzuri sana za kijasusi. Tulipata Wakenya wawili waliokuja na kufanya kazi na kundi la Kyagulanyi. Wao ni wataalamu wa vurugu. Tulipowakamata, tuliwaweka ndani ya friji kwa siku kadhaa,” alisema Rais Museveni.
Alisisitiza kuwa hawezi kuruhusu wageni “kuingiza Uganda katika machafuko” kama yale yaliyoshuhudiwa katika maandamano ya kizazi cha Gen Z nchini Kenya na vurugu za kabla na baada ya uchaguzi nchini Tanzania.
Alifichua kuwa viongozi wa Kenya, akiwemo Kinara wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Nje, Musalia Mudavadi, waliingilia kati kuhakikisha wanaharakati hao wanaachiliwa huru, ingawa yeye alitaka waendelee kuzuiliwa kwa muda mrefu zaidi.
Bw Njagi anayejulikana kwa jukumu lake katika maandamano ya Kenya ya Juni 2024, hapo awali alizuiliwa kwa siku 32 jijini Nairobi pamoja na wanaharakati wengine Longton Jamil na Aslam Longton.
Awali, Msemaji wa Polisi wa Uganda, Kituuma Rusoke, alikanusha taarifa za kuwa Wakenya hao wanazuiliwa Uganda. Hata hivyo, Rais Museveni alithibitisha kwamba wawili hao walikuwa miongoni mwa watu kadhaa wanaofadhiliwa na “makundi ya kigeni yenye wivu kwa maendeleo ya Uganda katika viwanda, uundaji wa ajira na amani.”
Alidai kwamba nguvu za nje zinajaribu kutumia Waganda “waliopoteza mwelekeo” na kufadhili vijana ili kusababisha vurugu.
“Tunazalisha bidhaa za viwandani na sasa tunakaribia kupata mafuta yetu. Wameingiwa na wasiwasi na sasa wanawafadhili vijana kufanya mambo mabaya,” alisema.
Rais Museveni, 81, ambaye anawania muhula mwingine, alisisitiza kuwa ataendelea kuwakamata wote wanaoonekana kuwa tishio kwa uthabiti wa Uganda. “Hatutakaa tu kutazama. Tutawakamata, na baada ya muda, tutawaachilia,” aliapa.
Rais Museveni pia alionya dhidi ya maandamano yenye vurugu, akiyarejelea yale ya mwaka 2020 yaliyosababisha vifo vya vijana kadhaa katika maandamano yaliyopangwa na upinzani. Alitaka wananchi kuonyesha kutoridhika kwa njia ya amani: “Mnaweza kwenda uwanjani Kololo na kuonyesha kwamba hamjaridhika, lakini msichome wala kuharibu mali.”