Maandamano yameivurugia TZ fursa za kupata mikopo -Samia
UWEZO wa Tanzania kupata ufadhili kutoka kwa taasisi za kimataifa huenda ukawa kibarua kutokana na maandamano yaliyosababisha vifo vya mamia waliojitokeza kupinga uhalali wa uchaguzi.
Kulingana na rais huyo, mchakato wa kupata ufadhili hautakuwa rahisi kwani nchi hiyo ‘ilitiwa doa’ na watu ambao hakuwataja.
Kiongozi huyo alisema hayo wakati wa kuapishwa kwa mawaziri wake aliowateua, akiwemo bintiye.
Makundi ya kutetea haki za binadamu, vyama vya upinzani na Umoja wa Mataifa wamesema kuwa huenda mamia ya watu waliuawa katika maandamano hayo ya vurugu, ingawa serikali inapinga takwimu hizo kuwa zimetiwa chumvi.
“Mara nyingi tunategemea nje, mikopo kutoka taasisi mbalimbali za kimataifa, benki za kimataifa, lakini yaliyotokea katika nchi yetu yameharibu jina la nchi yetu kidogo,” Samia alisema.
“Hilo linaweza kupunguza sifa yetu ya kupata mikopo hiyo kwa urahisi kama tulivyofanya katika muhula wetu wa kwanza…. kilichotokea kinaweza kuturudisha nyuma hasa kimaendeleo,” aliongeza.
Waangalizi wa Umoja wa Afrika walisema kura hiyo haikuwa ya kuaminika na kwamba walikuwa na lengo la kujaza masanduku ya kura.Serikali imepuuzilia mbali ukosoaji wa mchakato huo na kusema uchaguzi ulikuwa wa haki.
Samia ameahidi kuchunguza ghasia za uchaguzi na wiki iliyopita alitoa rambirambi kwa familia zilizofiwa, hali yake ya kukiri hadharani kuhusu machafuko hayo, ambayo yamesababisha mzozo mkubwa zaidi wa kisiasa nchini humo kwa miongo kadhaa.
Wakati wa kuapishwa kwa mawaziri hao katika jiji la Dodoma mnamo Novemba 18, 2025, aliwataka viongozi wajikite katika kutafuta fedha kutoka vyanzo vya ndani.
Mwezi Juni, wizara ya fedha ilisema ilipanga kukopa kutoka nje kima cha Sh468 bilioni katika mwaka wa fedha wa 2025/26 (Julai-Juni).
Katika bajeti yake ya mwaka wa kifedha wa 2024/25, iliweka ruzuku ya nje na mikopo yenye masharti nafuu iliyopangwa kuwa Sh5.13 trilioni.
Rais Samia aliwaambia mawaziri hao kuwa serikali yake imejipanga kurekebisha hali hiyo na kusisitiza kuwa sasa miradi ya maendeleo katika muhula wa pili wa serikali ya awamu ya sita itaanza kutekelezwa kwanza kwa kutumia mapato ya ndani.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa nchini Tanzania wanasema kuwa kauli ya Rais Samia inatoa ujumbe kwa wananchi kuwa hali ya kiuchumi itakuwa ngumu katika kipindi hicho cha muda.
Mchambuzi mmoja alisema, “Anatoa ujumbe wa moja kwa moja kuhusu uzito wa uchumi na anawaeleza wananchi wajikaze.”
Mabadiliko ya baraza la mawaziri yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan yamekuja katika kipindi ambacho serikali inakabiliwa na changamoto za kurejesha hali ya utulivu na kuimarisha uchumi baada ya kipindi cha misukosuko ya kisiasa yaliyosababisha vifo vya watu, majeruhi na uharibifu wa mali.