Waliokaidi kulipa mikopo ya HELB kuwindwa na polisi hadi vijijini
NA CECIL ODONGO
BODI ya Kutoa Mikopo kwa Wanafunzi wa Vyuo vya Juu (HELB), sasa itaanza kutumia polisi kuwaandama zaidi ya watu 74,000 hadi vijijini, ambao hawalipi pesa walizokopeshwa kufadhili elimu yao ya juu.
Kulingana na Waziri wa Elimu, Amina Mohamed, hatua hiyo itahakikisha HELB inakusanya deni lake la Sh7.2 bilioni kutoka kwa watu hao.
Akihutubu Jumatano, aliwengi wale hawalipi tayari wana kazi za kuwawezesha kulipa mikopo yao, lakini wamekuwa wakikataa kimakusudi.
“Nawaomba waajiri watafute mbinu za kuwashinikiza waajiriwa kulipa mikopo yao ili wanafunzi wengine waweze kunufaika. Tutaanza kushirikiana na maafisa wa usalama ili kuwakamata wafanyakazi wanaokataa kulipa mikopo yao kwa HELB,” akasema.
“Operesheni hii itawanasa hata wafanyakazi wa kampuni za huduma za mawasiliano ambao wameajiriwa kama wahudumu wa Mpesa, Airtel Money na kazi nyingine zinazoendelea kuibuka. Hatutavumilia vijisababu vyao kwamba mishahara yao ni midogo,” akasema Bi Mohamed.
Bodi hiyo Jumatano ilizindua mpango wa miaka mitano (2019-2023) wa kuboresha ufadhili kwa wanafunzi wa vyuo, ambapo ilitangaza inalenga kuongeza kiwango cha ufadhili kutoka Sh70 bilioni hadi Sh90 bilioni katika muda huo.
Afisa Mkuu Mtendaji wa HELB, Charles Ringera alisema bodi yake imewahudumia zaidi ya Wakenya laki nane kupata elimu ya juu katika muda wa miaka 24 iliyopita.
Wanafunzi wa vyuo vikuu nchini wamekuwa wakilalamika kwamba fedha kutoka kwa bodi hiyo ni kidogo mno.
Hata hivyo kiasi cha pesa zinazokopeshwa hakijaongezwa kwa muda mrefu licha ya kupanda kwa gharama ya maisha.