Taiwan, Japan zaungana kukabili China
TAIPEI, TAIWANI
RAIS wa Taiwan Lai Ching-te jana aliunga mkono Japan huku uhasama ukiendelea kutokota kati ya China na Japan kuhusiana na uhuru wa kisiwa hicho.
China mnamo Alhamisi ilisema kuwa itasitisha uagizaji wa bidhaa kutoka Taiwan kama sehemu ya mbinu yake kuilemaza kiuchumi.
Uhasama kati ya Japan na China ulipanda tena baada ya Waziri Mkuu wa Japan, Sanae Takaichi kusema kuwa wapo tayari kukabili China kijeshi iwapo itaivamia Taiwan.
Lai aliweka picha mitandaoni akila chakula cha mchana cha Japan na kutumia maelezo kwa lugha ya Kijapani.
“Chamcha cha leo ni sushi na supu ya miso,” akaandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Serikali ya Taiwan imekuwa ikisisitiza kuwa, nchi hiyo haitakubali kuwa chini ya uongozi wa China.
Miaka michache iliyopita, China ilizima uagizaji wa samaki na papai kutoka Taiwan. Hii ni miongoni mwa mbinu za China kuhakikisha kwamba Taiwan inalegeza kamba na kuwa chini ya himaya yake.
Jana, Waziri wa Masuala ya Nje wa Taiwan Lin Chia-lung alisema kuwa mbinu ya China kutumia udikteta wa kiuchumi na kijeshi kudhulumu mataifa mengine imepitwa na wakati na hawataikubali kamwe.