MUUNGANO wa Upinzani Novemba 20, 2025 ulikejeli hotuba ya Rais Rais William Ruto kuhusu Hali ya Taifa, ukimlaumu kwa kupuuza hasira za umma, kufumbia macho malalamishi ya waandamanaji wa Gen Z, na kutoa ahadi hewa.

Haya yalijiri huku Rais Ruto akisifu miaka yake mitatu madarakani kama kipindi cha mageuzi makubwa na kupuuza ukosoaji wa upinzani.

Katika taarifa iliyosomwa na Kiongozi wa Wiper Patriotic Front Kalonzo Musyoka, viongozi hao walitaja maandamano ya Gen Z ya Juni 2024 kama tukio la kihistoria ambalo Rais alishindwa kulikabili.

Walisema vijana waliojitokeza barabarani na mitandaoni hawakuwa watu wenye hasira tu, bali kizazi kilicholalamikia ufisadi, hali ngumu ya kiuchumi na utamaduni wa jeuri wa wanasiasa.

Upinzani ulimshutumu Rais kwa kupuuza malalamishi kuhusu gharama ya juu ya maisha, mchakato tata wa kuanzishwa kwa Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF), na Ushuru wa Nyumba, masuala yaliyosababisha maandamano ya kitaifa mwaka jana. Badala yake, walisema, hotuba yake ilijikita pakubwa katika kujisifu na kupuuza maisha halisi ya Wakenya wa kawaida.

“Gen Z walisema imetosha. Walikataa kukubali ahadi hewa’ kama njia ya kuongoza. Vijana wetu walikataa usimamizi mbovu wa SHA/SHIF uliowanyima wapendwa wao huduma za afya.

Wakenya kote walikataa ushuru wa nyumba ambao si chochote ila hazina ya siri; ufisadi wa hali ya juu,” Bw Musyoka alisema.

Upinzani pia ulimshutumu Rais kwa kutelekeza dira ya kitaifa ya Ruwaza ya 2030. Walidai mabadiliko hayo yamevuruga mipangilio ya maendeleo ya taifa, yamewaongezea Wakenya mzigo wa ushuru tata, na kuacha nchi bila mwelekeo thabiti wa kiuchumi.

“Hasa Wakenya walipinga usaliti wa Ruwaza ya 2030. Badala yake leo tuna ahadi na mipango hewa ya Ruto, ambayo leo utasikia ikisifiwa bungeni na mtu anayetamausha raia,” aliongeza.

Lakini Rais Ruto alipuuza ukosoaji huo akisema ni upotoshaji wa kisiasa. Katika hotuba yake aliutaja upinzani kama “makuhani wa unafiki” wanaokosoa bila kutoka suluhu mbadala.

“Kila mtu anaweza kusema anachotaka, na huo ndio uzuri wa demokrasia yetu,” alisema. “Lakini hakuna mtu aliye na haki ya kutengeneza uongo kwa maslahi binafsi na kuuza kama ukweli. Ukweli ndio niliowasilisha, wazi, unaothibitishwa na usiopingika.”

Upinzani pia ulitilia shaka hali ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), wakionya kuwa makamishna wapya “hawajaepuka ushawishi wa kisiasa na wameingia ofisini wakiwa na doa baada ya kupuuzwa kwa maafikiano ya NADCO.

“Hawajawahi kushauriana na upinzani kuhusu masuala muhimu ya uchaguzi na badala yake wamejigeuza kuwa tume inayotumikia maslahi ya Ikulu,” Bw Musyoka alisema.

Walisema kuwa mchakato unaoendelea wa usajili wa wapigakura unaweza kupotosha matokeo ya uchaguzi hata kabla ya siku ya kupiga kura. Walitaja kuanzishwa ghafla kwa utambuzi wa mboni za macho, muda mfupi wa usajili katika ofisi za maeneo bunge na udhaifu katika ulinzi wa data.

“Uchaguzi hauhitaji kuibwa siku ya kupiga kura,” Bw Musyoka alionya. “Unaweza kuibwa kimyakimya wakati wa usajili ambapo uangalizi ni hafifu.”