Mkanganyiko kuhusu karo ya wanafunzi wa Gredi 10
WAZAZI ambao watoto wao wanatarajiwa kujiunga na shule za Sekondari Pevu wataendelea kuchanganyikiwa kuhusu kiwango cha karo ambacho watahitajika kulipa kuanzia Januari 2026.
Hii ni baada ya Waziri wa Elimu Julius Ogamba kukana kwamba wanafunzi wote watakaosomea shule za mabweni watahitajika kulipa karo Sh53,554 kila mwaka.
Kiasi hicho cha karo, kilitajwa kwenye mwongozo kuhusu mpito hadi Shule ya Sekondari ya Pevu uliotolewa na Wizara ya Elimu Jumanne, Novemba 4, 2024.
Aidha, mwongozo huo unaondoa uainishwaji wa shule kwa misingi ya Shule za Kitaifa, Shule za Mikoa na Shule za Ngazi ya Kaunti.
Isitoshe, mwongozo huo unasema kuwa wanafunzi watakaosomea katika Shule za Upili za Kutwa watahitajika kulipa Sh9,374 kila mwaka, tofauti na ilivyo sasa ambapo hawatozwi karo yoyote.
“Karo itakayotozwa katika viwango vyote vya shule zote za mabweni za Sekondari Pevu itasalia Sh53,554 kila mwaka kulingana na Ilani kwenye Gazeti Rasmi la Serikali Nambari 1555 la Machi 10, 2015,” ikasema mwongozo huo uliotolewa na Wizara ya Elimu.
Wakati huu, wazazi ambao watoto wao wanasomea shule za upili za kitaifa wanalipa Sh53,554 kila mwaka ilhali wale wanaosomea katika shule za kimkoa na kaunti wanalipa Sh40,535.
Ikiwa shule zote zitalipishwa karo ya Sh53,544 ina maana kuwa wanafunzi watakaojiunga na shule ambazo zamani zilianishwa kama shule za hadhi ya kimkoa na kaunti, watalipa karo ya juu kuliko ya sasa.
Lakini kwenye taarifa Alhamisi, Novemba 6, 2025, Waziri Ogamba alitoa taarifa akisema Wizara yake haijapandisha karo katika shule za mabweni.
“Wazazi, wanafunzi na umma kwa ujumla unajulishwa kwamba hamna mabadiliko yaliyofanywa kwa karo ya shule za mabweni au aina nyingine ya ada zinazohitajika kulipwa na wanafunzi. Mwongozo wa sasa kutoka kwa Wizara ya Elimu kuhusu karo inayohitajika kulipwa katika shule za mabweni utaendelea kutumika,” Bw Ogamba akaeleza kwenye taarifa hiyo aliyoituma kupitia kaunti yake ya mtandao wa X.
Alipuuzilia ripoti kuhusu mwongozo mpya uliotolewa na Wizara yake iliyochapishwa katika baadhi ya vyombo vya habari Alhamisi, Novemba 6, 2025.
Hata hivyo, Bw Ogamba hakukana kwamba mwongozo uliorejelewa katika taarifa za vyombo vya habari haukutolewa na wizara.
Hii ndio maana wazazi ambao wanafunzi wao walifanya mtihani wa kitaifa wa Gredi ya 9 mwezi jana, watachanganyikiwa kuhusu ni upi msimamo halisi wa Wizara ya Elimu kuhusu kiasi cha karo ambacho watoto wao watahitajika kulipa watakapojiunga na Shule za Sekondari Pevu, Januari, 2026.
Huku Waziri Ogamba akisema kuwa serikali itaendelea kutoa Sh22, 224 kila mwaka kwa wanafunzi wa Shule za Sekondari Pevu, mwongozo kutoka wizara yake unasema serikali itatuma Sh12,870, kila mwaka, kwa kila mwanafunzi katika shule za kutwa na zile za mabweni.
Kwa upande mwingine, serikali itatuma Sh32, 600 kwa shule za wanafunzi wanaishi na ulemavu.