Mbadi asema anatosha mboga kurithi Raila
WAZIRI wa Fedha, John Mbadi amesema yuko tayari kuongoza jamii ya Waluo kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu hayati Raila Odinga.
Bw Mbadi pia amesema kuwa anastahili kuwa msemaji mkuu wa kisiasa wa jamii hiyo.
Ingawa alikiri hakuna anayeweza kuvaa viatu vya Odinga kikamilifu, Bw Mbadi alisema anaelewa njia ya kisiasa aliyotembea kiongozi huyo wa ODM, lakini hatatumia mtindo wake bali atachonga mbinu yake mwenyewe kuongoza .
Kauli yake inajiri wakati jamii ya Waluo inapambana na suala la kusaka mrithi wa Odinga.
Kulingana na Bw Mbadi, safari ya kisiasa ya zaidi ya miongo mitatu ya Odinga haiwezi kurudiwa.
“Ninajua mahali Raila alitaka kutupeleka, na njia alizokuwa akifuata. Hata hivyo, sitavaa viatu vyake; nitanunua viatu vinavyonifaa na nitaiongoza jamii ya Waluo kwa njia ninayoijua, tunapoingia Canaan,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Raila Odinga alibeba mwenge na akaongoza jamii yetu kwa zaidi ya miaka 30. Alipanga kutupeleka Canaan lakini, kwa bahati mbaya, hakuweza kutufikisha. Hata hivyo, lazima tuingie Canaan,” alisema Bw Mbadi katika hafla ya uwezeshaji Kisumu iliyofanyika Ijumaa.
Alipuuzilia mbali madai kwamba mtu yeyote anaweza kuchukua nafasi ya Odinga bila kupitia misukosuko ya kisiasa aliyopitia marehemu kiongozi huyo wa ODM.
“Watu wengine wanasema tuingie katika viatu vya Raila, lakini ukweli ni kwamba hakuna anayeweza. Ukivivaa lazima ufungwe miaka kadhaa,uteswe na kura zako ziibwe mara kadhaa,” alisema.
Akimfananisha Odinga na Musa wa Biblia aliyeongoza watu wake lakini hakuwahi kuingia nchi ya ahadi, Bw Mbadi alisema jamii ya Waluo lazima iingie nchi hiyo chini ya uongozi wake.
“Raila Odinga alikuwa kama Musa. Alionyeshwa Canaan lakini hakuingia. Lakini sisi lazima tuingie Canaan,” aliongeza.
Kauli yake inajiri chini ya mwaka mmoja baada ya mjane wa Odinga, Ida Odinga, kumtaja hadharani kama kiongozi anayefaa kuongoza jamii ya Waluo baada ya Raila.
Ida alisema Mbadi amekomaa kisiasa na yuko kwenye nafasi bora zaidi kuongoza jamii hiyo yenye ushawishi mkubwa.
Alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya Raila kutangaza kuwania uongozi wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).
Akimtaja Bw Mbadi, Ida alisema kushirikiana kwake kwa muda mrefu na Raila kunamweka mbele ya wandani wengine.
“Kabla sijaondoka nyumbani kwenda Nyandiwa, Baba aliniambia niwaletee salamu. Alisema msitetereke kwa mabadiliko ya kisiasa, maana tayari ameunda timu madhubuti ya kuchukua usukani akienda Addis Ababa,” alisema Ida.
Aliongeza: “Kwa muda mrefu Baba amekuwa akimfundisha Mbadi. Hahitaji mafunzo zaidi. Unatosha. Mbadi Nyang’. Mbadi ndiye aliye moyoni mwa Raila.”
Viongozi wengine wanaotajwa katika mchuano wa urithi ni Oburu Oginga, Waziri wa Kawi na Petroli Opiyo Wandayi, Gavana wa Siaya James Orengo, Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga.
Vijana wanaojipanga kwa nafasi za baadaye ni Winnie Odinga na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino.
Kwa upande mwingine, Bw Mbadi alisihi ODM kuzingatia kurejea mamlakani, akisema chama hakiwezi kuendelea kujihusisha na maandamano pekee.
“Hakuna chama cha kisiasa kinachoanzishwa kuwa kwenye barabara. Hakuna chama cha kisiasa kinachoanzishwa kufanya maandamano kila wakati.Vyama si mashirika ya kiraia,” alisema.
Alisisitiza kuwa ODM lazima ipange malengo ya wazi ya uchaguzi wa miaka ijayo.
“Ikiwa hatuwezi kutoa rais wa Kenya 2027, basi lazima tutoe rais 2032. Hilo ndilo sharti la chini kabisa kwa ODM na kwa jamii yetu,” aliongeza.
Aliwakosoa wanaopinga serikali jumuishi, akisema“Vyama vya siasa huundwa kuunda serikali. Lazima tujipange. Lazima tujifunze kuwa serikalini. Wale wanaotuambia tusishirikiane na William Ruto, eti tushirikiane na Rigathi Gachagua au Kalonzo, katika mipango yao sisi hatupo.”