Habari

Ruto, Museveni waahidi kupeleka SGR hadi DRC

Na CECIL ODONGO November 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto ametangaza kuwa reli ya kisasa ya SGR sasa itajengwa kutoka Naivasha-Kampala hadi Rwanda na kwenye mpaka wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) kuanzia mapema mwaka ujao.

Dkt Ruto alisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha biashara za ukanda huu hasa Uganda na Kenya na Jumuiya nzima ya Afrika Mashariki.

“Januari tutazindua ujenzi wa SGR kutoka Naivasha hadi Kampala na itaungana na ile ya Malaba-Kampala na baadaye DRC,” akasema Rais.

Alikuwa akiongea katika eneo la Osukuru, Wilaya ya Tororo Uganda ambapo pamoja na Rais Yoweri Museveni walizindua mradi wa Kiwanda cha utengenezaji wa chuma, Devki.

Rais Ruto alisema SGR itakuwa mradi wa pamoja na utazinduliwa Januari 2026.
Wakati huo huo, Rais alisema kuwa Kenya na Uganda zitaongeza mfumo wa usafirishaji wa mafuta kupitia mabomba hadi DRC.

Rais Ruto pia alisema uhusiano wa Kenya na Uganda ni imara na nchi hizo zilibuni mbinu mpya ya kuimarisha uchumi wao katika kikao cha mawaziri wao Nairobi hivi majuzi.

Rais Museveni naye alisema miradi ya kiviwanda itakuwa na manufaa tu wakati ambapo jamii zitapata nafasi za ajira.

Mwenyekiti was Devki Nerendra Ravel alihakikishia marais hao kuwa kiwanda hicho kitawategemea na kuwatumia wafanyakazi kutoka Uganda.

Aliahidi kuwa mradi huo utabuni nafasi 15,000 za ajira kwa raia wa Uganda.
“Naihakikishia jamii ya hapa kuwa asilimia 90 ya kazi itafanywa na watu wa hapa,” akasema Dkt Raval.