Habari

Oburu naye awapangia wapinzani, sasa aungwa na wanasiasa wakali

Na MOSES NYAMORI November 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KINARA mpya wa ODM Dkt Oburu Oginga amegutuka na kuanza kujijenga upya kisiasa huku akibuni kundi la wanasiasa maarufu kama wandani wake.

Mikakati ya Dkt Oginga, nduguye marehemu Kiongozi wa ODM Raila Odinga, inalenga kuwazima wanasiasa chipukizi ambao wameibuka kumpinga na sasa wanashinikiza aondolewe.

Dkt Oginga anapambana na maasi ya ndani kwa ndani ya ODM ambayo yanaendelezwa na kundi la wabunge pamoja na bintiye Raila, Winnie Odinga.

Kando na Bi Winne ambaye ni Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) wanasiasa wengine wanaompinga Dkt Oginga ni Mbunge wa Saboti Caleb Amisi na mwenzake wa Embakasi Mashariki Babu Owino.

Wanasiasa hao wanasukuma Kongamano la Kitaifa la Chama (NDC) liandaliwe ili wanachama wa ODM wawachague viongozi wapya.

“Iwapo kiongozi wa chama atalemewa kutekeleza majukumu yake kutokana na sababu za kiafya, mauti, kujiuzulu ama akiondoka chamani, NDC itaandaliwa kumchagua kiongozi mpya wa chama,” inasema kifungu cha 6.2 cha Katiba ya ODM kuhusu uchaguzi wa maafisa wa kitaifa.

Kupambana na wabunge hawa chipukizi Dkt Oginga ana Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi, Magavana Abdulswamad Nassir (Mombasa), Gladys Wanga (Homa Bay) na Simba Arati wa Kisii. Mabw Arati na Nassir ni manaibu wa Dkt Oginga huku Bi Wanga akiwa mwenyekiti wa chama.

Pia kwenye kundi lake ni Kiongozi wa Wengi Junet Mohamed na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kisumu Ruth Odinga, dadake Dkt Oginga kisha Elijah Oburu naye sasa ni msaidizi wa kibinafsi wa babake.

“Mimi ndiye nilipendekeza jina lake wakati wa mkutano wa Kamati Kuu ya Chama mnamo Oktoba 16 na baadhi ya watu wanaozungumza huko nje waliunga hilo,” akasema Bw Nassir kwenye mahojiano na Taifa Leo Dijitali.

Uteuzi wa Dkt Oginga ulithibitishwa mnamo Novemba 16 wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya ODM kule Mombasa.

“Hatutawaruhusu wasambaratishe chama kwa sababu tunajua wanatumiwa. Kwa sasa Dkt Oginga ndiye kiongozi na wanaomsumbua sasa ndio wale ambao walimpa Raila wakati mgumu alipotia saini makubaliano ya kushirikiana na Rais William Ruto,” akaongeza.

Bw Wandayi naye ni kati ya wanasiasa ambao wanaamini uongozi wa Dkt Oginga akisema ana malengo na sifa za uongozi sawa na za Raila.

“Hili eneo litasalia nyuma ya Oburu Odinga,” akasema Bw Wandayi hivi majuzi akiwa Kaunti ya Siaya.