Natembeya, Khalwale walia baada ya kupokonywa walinzi kuelekea uchaguzi mdogo Malava
GAVANA wa Trans Nzoia George Natembeya na Seneta wa Kakamega Boni Khalwale sasa wamelaumu serikali kwa kuwapokonya walinzi katika mazingira tata, siku moja kabla ya uchaguzi mdogo wa Malava, hali ambayo imeongeza joto la kisiasa.
Natembeya alisema Jumatano kuwa maafisa wake wote sita wa ulinzi — wakiwemo maafisa wa GSU na dereva wake — waliamriwa kuripoti katika vituo vya polisi usiku wa manane bila maelezo yoyote.
“Wamewaondoa wote, sina hata mmoja nyumbani au ofisini. Kwa nini? Mimi sijui. Uliza Ruto,” akasema gavana huyo, akidokeza uwezekano wa kuandamwa kisiasa kwa msimamo wake mkali dhidi ya serikali.
Gavana huyo alisema kulingana na kiwango cha vitisho alivyopitia, ikiwemo tukio la kushambuliwa kwa risasi Jumamosi, angepaswa kuongezewa ulinzi na sio kupunguzwa.
Wachambuzi wa siasa wanahusisha hatua hiyo na jitihada za kumtisha kabla ya uchaguzi wa kesho, ambapo Natembeya amekuwa akimfanyia kampeni mgombea wa upinzani Malava.
Lakini gavana huyo amesema hatatishika. “Hawawezi kuninyamazisha katika mapambano dhidi ya utawala mbaya na ukombozi wa watu wangu,” akaongeza.
Katika tukio linalofanana, Seneta Boni Khalwale alidai Jumatano kuwa walinzi wake waliondolewa bila taarifa, na kwamba kuna mpango wa kumkamata nyumbani kwake kabla ya kura kuanza kupigwa.
“Kuna njama ya kuniweka ndani na kunizuilia kabla ya uchaguzi,” akasema, akidai polisi wanapanga kumkamata ili kumtisha.
Haya yanajiri huku mgombea wa upinzani katika kiti cha Malava, Seth Panyako, naye akitoa madai mazito kuwa kuna njama ya kukamata viongozi wakuu wa upinzani akiwemo George Natembeya, Eugene Wamalwa, Khalwale na yeye mwenyewe.
Katika taarifa kupitia X (zamani Twitter), Panyako alidai kuwa serikali inapanga kutumia polisi kutisha wapiga kura na kuhujumu uchaguzi.
“Wamepanga kutunyanyasa ili kuiba uchaguzi ambao tayari wamepoteza,” akasema.
Aliongeza kuwa viongozi kadhaa wa eneo hilo akitaja Mbunge wa Lugari Nabii Nabwera, Rashid Echesa na msaidizi wa Rais Ruto, Farouk Kibet, wanapanga vurugu katika wadi mbalimbali za Malava.
Bw Panyako alizitaka taasisi za usalama “kuwazuia” wanaopanga ghasia na kuhakikisha hakuna vifo vinavyoweza kutokea.
Jana, waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen alikiri kwamba walinzi wa viongozi hao waliondolewa.akidai kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kulingana na tathmini za usalama.
Murkomen, akizungumzaalisema hatua ya kuondoa au kubadilisha walinzi wa viongozi ni jambo la kawaida linaloamuliwa na idara za usalama, na si la kisiasa kama inavyodaiwa..
“Kwa kweli, si Natembeya pekee. Kuna viongozi wengine ambao walinzi wao pia wameondolewa.. Lakini pia kuna maafisa wanaoenda kinyume na sheria na kutumia vibaya mamlaka yao. Serikali haitakubali,” alisema Murkomen.
Alisisitiza kuwa hakuna kiongozi anayepokonywa walinzi ili kumtisha kisiasa, bali mabadiliko yoyote yanatokana na makadirio ya viwango vya hatari.