KATAMBE! Leo ni leo katika chaguzi ndogo
LEO, Novemba 27, 2025, wapiga kura katika maeneo 24 ya uchaguzi wanatarajiwa kupiga kura katika uchaguzi mdogo unaoonekana kuwa na athari kubwa kisiasa, na kuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Pande zote mbili, Serikali Jumuishi chini ya Rais William Ruto na Muungano wa Upinzani unaoongozwa na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua, zipo katika kinyang’anyiro hiki ili kujenga umaarufu wa kisiasa.
Tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) iliyoundwa upya pia inamlikwa ikiwa ni uchaguzi wake wa kwanza wa kiwango kikubwa ambao tayari umegeuka kuwa chanzo cha mvutano wa kisiasa na shaka kutoka kwa umma.
Ingawa uchaguzi huu ni mdogo, umeibua hisia ukifuatiliwa kitaifa, ambapo vyama vinavyoshindana vimepeleka viongozi wakuu na rasilmali nyingi mashinani.
Ripoti za ghasia, kuhongwa kwa wapiga kura na madai ya udanganyifu zimeongeza shinikizo, na kufanya uchaguzi huo kuwa mtihani muhimu kwa IEBC.
Matokeo ya uchaguzi pia yatajenga heshima kwa upande utakaoshinda, na kuufanya kuvutia ushirikiano mpya kabla ya uchaguzi ujao. Pia yanatarajiwa kuwa kipimo cha kuchagua washirika wapya wa kimkakati, ikiwemo makubaliano kabla ya uchaguzi.
Mbali na wagombea 181 walio kwenye kinyang’anyiro cha kura, matokeo ya uchaguzi mdogo wa leo pia yataathiri au kuimarisha nguvu za kisiasa za viongozi wa kikanda.
Kutakuwa na uwezekano wa kuibuka kwa wanasiasa wapya wenye nguvu huku baadhi ya viongozi wa zamani wakififia.
Viongozi wakuu ambao umaarufu wao utajaribiwa katika uchaguzi huu mdogo ni pamoja na Makamu wa Rais Kithure Kindiki, Mkuu wa Waziri Mkuu Musalia Mudavadi, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, mwenzake Seneti Amason Kingi, Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na Mwenyekiti wa Taifa wa ODM na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga.
Matokeo mabaya katika viti vya kimkakati kama vile Mbeere North, Malava, Kasipul, Ugunja na Magarini yanaweza kumlazimisha Rais Ruto kurekebisha ushirikiano wake.
Viongozi wa upinzani kama Gachagua, Kalonzo Musyoka na wengine pia watatumia matokeo haya kugawana nyadhifa katika muungano wao mpya kuelekea 2027.
Kwa Prof Kindiki, ambaye nyumbani kwake kijijini ni umbali wa kilomita 21 kutoka Mbeere North, kushindwa kutamaanisha kupoteza hadhi yake kama kiongozi mpya wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya.
Pia kutakuwa ishara ya mabadiliko makubwa ya kisiasa katika eneo lililoingia Ruto madarakani mwaka 2022.
Prof Kindiki anaunga mkono mgombea wa UDA Leonard Muthende, huku Gachagua akiunga mkono Newton Kariuki maarufu kama Karish wa Democratic Party (DP).
“Viongozi kote wanachukulia uchaguzi mdogo kama kipimo cha nguvu za kisiasa. Hapa Kenya, unaunda mtazamo wa nguvu kwa viongozi waliopo na wapinzani wao. Kushindwa kwa UDA ni ushindi kwa Gachagua, kuonyesha Ruto alikosea kumtema,” anasema Prof David Monda, mtaalamu wa masuala ya kisiasa.
Anasema matokeo yana maana kubwa. Ikiwa Kindiki atasaidia mgombea wa UDA kushinda Mbeere North, hadhi yake ya kisiasa itaongezeka.
Vivyo hivyo Mudavadi na Wanga ambao wataimarika zaidi katika mpango wa Ruto wa kuunda kikosi cha uchaguzi wa 2027. Kushindwa katika uchaguzi mdogo huu ni aibu kubwa kwa Ruto na kutaimarisha kampeni ya “Wantam”.
Katika Kasipul, hali ya kisiasa imechemka, na mitazamo ya wakazi inaonyesha kuwa ushindi unaweza kuelekea upande wowote baada ya miezi kadhaa ya kampeni nzito kati ya wagombea wawili wanaoongoza – Boyd Were wa ODM na Philip Aroko (Huru).
Ingawa jumla ya wagombea ni 10, kinyang’anyiro kimebaki kati ya wawili hao. Eneo hilo lina jumla ya wapiga kura 67,513.
Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga ameongoza kikosi cha ODM katika kampeni zilizoonekana kutumia rasilmali nyingi na kuhusisha vigogo wa chama.
Kwa kawaida, kampeni Kasipul zingekuwa rahisi kutokana na ngome ya muda mrefu ya chama hicho, lakini hali imebadilika.
Katika Banisa, Kamishna wa IEBC Hassan Norr Hassan alisema mipango yote ya uchaguzi mdogo imekamilika na vifaa vimepelekwa katika vituo vyote 81 katika kata tano za eneo hilo.
“Tuko tayari kwa zoezi la Alhamisi ambapo wakazi wa Banisa watawachagua mbunge wao,” alisema.
Polisi pia wamesema kuwa usalama umeimarishwa, kila kituo kikiwa na angalau maafisa wawili na wengine wakiwa doria.
Katika Magarini, wakazi hatimaye wanapata fursa ya kumchagua mwakilishi wao baada ya kukaa karibu miaka miwili bila mbunge kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Juu Mei 2024 uliobatilisha ushindi wa Harrison Kombe.
Uchaguzi mdogo una wagombea tisa, akiwemo Kombe (ODM), Stanley Kenga (DCP), Furaha Chengo Ngumbao (DNA), Hamadi Chadi Karisa (RPK), na John Sulubu Masha (Kenya Social Congress).
Wengine ni Emmanuel Kitsao Kalama (TWAP), mgombea huru Amos Katana, Sarah Wahito Gakahu (Kenya Moja Movement), na Jacob Themo Kwicha (FPK).
Katika Baringo, IEBC imetangaza vituo vipya vitatu vya kupigia kura kufuatia mafuriko yaliyomeza vijiji. Vituo vya Noosukro, Lake Baringo Secondary na Ng’ambo Primary vilihamishwa hadi vijiji vya Sokotei, Kipkimilwa na Kiserian.
Wagombea ni pamoja na Vincent Chemitei (UDA), Benjamin Chebon (TND), Shadrack Kibet Kaplawat (ARC), Steve David Kipruto (RLP), Samuel Letasio (KMM) na Daniel Kirui (UMP).