Rais wa Guinea-Bissau aendelea kuzuiliwa baada ya wanajeshi kupindua serikali
BISSAU, GUINEA-BISSAU
KUNDI la wanajeshi linaendelea kushikilia mamlaka Guinea-Bissau baada ya kumbandua uongozini Rais Umaro Sissoco Embalo mnamo Jumatano.
Wanajeshi hao walitwaa mamlaka siku moja kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya urais yaliyokuwa na ushindani mkali nchini humo.
Kupitia taarifa iliyosomwa na Msemaji wao Diniz N’Tchama, wanajeshi hao walisema wamebuni kituo kikuu cha kutoa amri ya kijeshi kuhakikisha taifa hilo linasalia thabiti.
Walisisitiza kuwa watasimamia nchi hiyo lakini hawakutaja muda ambao watakuwa usukani.
Aidha, hawakueleza wazi iwapo Embalo anazuiliwa, japo duru zilieleza kuwa alikuwa akizuiliwa nyumbani kwa mmoja wa wakuu wa jeshi.
Kwenye video ambayo ilienea sana mitandaoni, Fernandos Dias, ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa Embalo, alikuwa huru baada ya wanaume waliojihami kujaribu kumteka nyara.
Dias, alisema kuwa Waziri Mkuu wa zamani Domingos Simeos Pereira ambaye alishindwa na Embalo mnamo 2019 bado alikuwa akizuiliwa.
“Tumekuwa tukilengwa kwenye mapinduzi hayo kwa sababu nilishinda uchaguzi. Haya mapinduzi ni ya kutuzuia kuchukua mamlaka,” akasema.
Muungano wa Kiuchumi wa Mataifa ya Ukanda wa Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) ulikemea mapinduzi hayo na kusema kuwa maafisa wanaohusika na mchakato wa uchaguzi nao pia walikuwa wamekamatwa huku akitoa wito waachiliwe.
Guinea-Bissau ni taifa dogo la pwani ya mpaka wa Senegal na Guinea.
Mara nyingi kokeni inayopelekwa Ulaya hupitishwa kwenye taifa hilo dogo.