Jinsi msanii Lava Lava alivyowateka wakazi wa Lamu na shoo kali
MSANII wa Bongo Flava Abdul Juma Idd, almaarufu Lava Lava, amekuwa akisalia kwenye midomo ya wengi, akisifiwa kila anapofika kisiwani Lamu kutumbuiza hadhira.
Mara ya kwanza kufika kisiwani Lamu kupiga shoo ilikuwa Novemba 2022 wakati wa Tamasha la awamu ya 20 la Utamaduni wa Lamu.
Ni wakati akitumbuiza mamia ya mashabiki wake eneo la Mkunguni ambapo alichukua fursa hiyo kumtambulisha rasmi mpenzi wake mzungu kwa mara ya kwanza jukwaani.
“Nimesumbuka sana nikitafuta penzi. Nimeudhiwa na kuteswa kwa miaka mingi lakini nashukuru mwishowe nimempata kipenzi changu. Nachukua fursa hii kumtambulisha wangu wa moyo nimpendaye, mrembo kutoka nchi ya Macedonia. Karibu mpenzi wangu uwapungie mashabiki mkono,” alisema Bw Lava Lava huku akimshika mkono na kumsimamisha mrembo mzungu na kukatika naye jukwaani kuonyesha mahaba waliyonayo.
Tukio hilo liliwaacha mashabiki wengi wakimfurahia Lava Lava.

PICHA|KALUME KAZUNGU
Hata baada ya kurudi kwao Tanzania, gumzo zilisheheni mitaani mwa mji wa kale wa Lamu kuhusiana na kile mashabiki wa Bongo Flava walichodai ni kuvishwa hadhi ya juu na msanii wao.
“Waonaje msanii wa hadhi ya juu kama Lava Lava afiche uhusiano wake hadi kufika Lamu ndipo amtambulishe kipenzi chake kwa mara ya kwanza kwa umma? Hilo ni dhihirisho tosha kwamba Lava Lava anatuthamini sisi mashabiki wa Lamu si haba,” akasema Bw Omar Alwy.
Hatua hiyo iliwasukuma mashabiki wa Bongo Flava mwaka huu kuishinikiza serikali ya kaunti ya Lamu kumrudisha tena Lava Lava kuwatumbuiza kwenye Tamasha la awamu ya 23 la Utamaduni wa Lamu lililokamilika Jumamosi usiku.

Ni wakati wa tumbuizo za mwaka huu eneo hilo hilo la Mkunguni ambapo Lava Lava pia aliiteka upya mioyo ya mashabiki wake pale alipoisifu Lamu kwa kuwa na hoteli nadhifu na zenye maji safi kiasi cha msanii huyo kudai anaweza kunywa hata ya chooni.
“Nimependezwa na kila kitu Lamu. Niwaambie kitu? Hoteli niliyokuwa nakaa ina maji safi na salama. Naweza kunywa hata ya chooni. Tupige kelele kwa gavana wetu, Issa Timamy kwa kazi safi,” akasema Lava Lava huku akishangiliwa na kuinuliwa mikono na mashabiki wake.
Baadaye alifuatiliza kauli yake kwa kumwelekeza DJ kuuporomosha wimbo wake wa ‘Maji’ huku akibadili baadhi ya maneno ndani ya wimbo na kujaza jina ‘Lamu’ katikati yake.
Ni jambo lililowafanya mashabiki wa kisiwa cha Lamu kuvutiwa zaidi na hulka ya msanii huyo waliyedai hana maringo kama wengine wenye hadhi sawa na yake.
Kauli nyingine iliyowafurahisha mashabiki ni pale gavana wa Lamu alipofika jukwaani usiku wa manane, ambapo aliwaamkua mashabiki na kisha kumkaribisha rasmi Lava Lava Lamu.
Wakati akikaribishwa, Lava Lava alimuomba gavana amkubali kutafuta mrembo Lamu aoe na aishi kabisa hapo, hali iliyomwacha gavana Timamy na hadhira yote ikiangua kicheko cha furaha.
Baadaye Bw Timamy, akiwa ameandamana na viongozi wengine, ikiwemo katibu mkuu wa chama cha UDA na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Hassan Omar, Mbunge wa Matuga, kaunti ya Kwale, Bw Kassim Tandaza na wengineo waliwekewa kibao cha Lava Lava kwa jina ‘Desh Desh’ na kusakata densi jukwaani kwa dakika kadhaa kabla ya kumpisha msanii huyo kuendeleza shoo yake.
“Lava Lava hoyee. Ni raha si raha. Mumefurahi hamkufurahi? Tulipokualika kwa mara ya kwanza 2022, uliwaimbia vizuri watu wangu na ndiyo sababu tukakurudisha tena mwaka huu kwa sababu yao. Tunakushukuru kwa kuja na tunazidi kukukaribisha Lamu. Hata ukiwa huji kuimba wewe njoo utembee pia,” akasema Bw Timamy.

Naye Lava Lava alidandia, “Asante sana gavana wangu. Ningetaka pia na mke nioe kabisa hapa.”
Ni kauli iliyofurahisha hadhira kiasi cha warembo wengi kumkaribia msanii huyo jukwaanina kumpa mikoni katika kile kilichoonekana kujaribu kunadi sera za mapema mapema za kutaka nafasi ya posa kwake.
Baadhi ya waliohojiwa walidai hawaoni shida endapo ataoa Lamu na hata kujitafutia makao ya kudumu kwenye kisiwa hicho ambacho ni ngome ya dini ya kiislamu.
“Hatujali hata endapo Lava Lava ana mchumba au mke. Sisi dini yetu ya Kiislamu inakubali wake hadi wanne. Akituposa kwa nini tukatae ilhali tupo singo,” akasema Bi Halima Omar.
Lava Lava mwaka huu pia alitumbuiza hadhira ya kisiwa cha Lamu kwa muda mrefu zaidi wa zaidi ya masaa mawili unusu kinyume na 2022 ambapo alifika jukwaani na kupiga shoo kwa saa moja unusu pekee.
Jumamosi, Lava Lava alipanda jukwaani saa tano unusu usiku, ambapo alitumbuiza hadi saa nane alfajiri kabla ya kusepa.
Mamia ya mashabiki waliojitokeza walitumbuizwa kwa nyimbo wanazozienzi kama vile Ng’ari Nga’ri, Desh Desh, Gundu, Basi Tu, Wale Wale, Dede, Tuachane, Warembo, Kilio, Bado Sana miongoni mwa zingine.
“Ninawapenda sana mashabiki wangu, wanangu wa Lamu. Nitatafuta nyumba niishi hapa na nyinyi.Nyinyi ni watu wazuri,mpo na warembo wazuri na viongozi wema. Pongezi kwa gavana Timamy, baba na kipenzi chetu kwa maendeleo.Sitaacha kuja hapa,” akasema Lava Lava kabla ya kushuka jukwaani na kuondoka.

Mashabiki waliotumbuizwa hawakuficha furaha yao.
Biti Salim alishikilia kuwa hata iwe mara ngapi wapo tayari kumkaribisha msanii huyo kisiwani kuwatumbuiza.
“Yeye hana maringo kama wasanii wengine. Amedhihirisha upenda wake wa dhati kwa Lamu na watu wake. Tutasukuma arudi tena na tena hapa kisiwani. Hata kama itamaanisha kila mwaka,” akasema Biti Salim.
Bw Samson Kithi kutoka Malindi,kaunti ya Kilifi alikiri kuguswa na jinsi Lava Lava alivyowacharazia shoo ya kukata na shoka Lamu.
“Nilitoka Malindi kuja hapa Lamu baada ya kusikia Lava Lava atatumbuiza hapa. Sijuti kufika Lamu kushuhudia tumbuizo ya msanii huyo. Ametufurahisha sisi mashabiki wake kindakindaki,” akasema Bw Kithi.
Mbali na Lava Lava, wasanii wengine wa Bongo Flava waliowahi kufika Lamu kutumbuiza wakati wa maadhimisho ya Tamasha la Utamaduni ni Yasirun Yassin Shaban, anayetambulika jukwaani kama Yammi na mwenzake Dennis Mwasele, kwa jina la muziki D Voice (2024).
Wengine ni Sharif Said Juma, jina la jukwaani akifahamika kama Jay Melody (2023) na Mbwana Yusuf Kilungi kwa jina lingine Mbosso Khan (2019).