ODM yang’aa katika ngome zake Gachagua akipata kitu
Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kimejinyakulia ushindi muhimu katika chaguzi ndogo za Novemba 27, 2025, bila uwepo wa mwanzilishi wake Raila Odinga aliyefariki Oktoba 15.
Wakati huo huo, chama kipya kinachohusishwa na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua kimeanza kutoa ishara ya mabadiliko ya siasa za Kenya kwa kushinda viti kadhaa vya udiwani katika chaguzi hizo.
Katika eneo bunge la Kasipul, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilimtangaza Boyd Ongondo Were wa ODM kuwa Mbunge mpya baada ya kupata kura 16,819.
Mshindani wake wa karibu, mgombea huru Philip Nashon Aroko, alipata 8,476 katika kinyang’anyiro kilichokuwa na wagombeaji 10.
Ushindi wa ODM Kasipul ni muhimu kwa chama hicho hasa baada ya kifo cha Raila na unaonyesha kingali imara katika ngome yake ya Nyanza. Chama hicho kilishinda kwa urais uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Ugunja ambapo Moses Omondi alipata ushindi wa kishindo kwa kura 9,227.
Mgombea wa Wiper, Orodi Odhiambo, alifuatia kwa mbali na kura 1,819, huku Fredrick Ochiel wa UDM akipata 1,200. Kasipul na Ugunja yanapatikana katika ngome ya Raila ya Nyanza.
Ushindi huu mkubwa unatarajiwa kuimarisha misingi ya ODM katika ngome hiyo lakini bado unakuja wakati chama kinakabiliwa na maswali kuhusu mustakabali wake bila ushawishi wa moja kwa moja wa Raila.
Wakati ODM ikidumisha uthabiti wake katika ngome yake upande mwingine wa siasa umeanza kupata uwepo mpya.
Katika uchaguzi mdogo wa wadi ya Narok Town, Douglas Masikonde wa Democracy for the Citizens Party (DCP)chama kinachohusishwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachaguaalitangazwa mshindi kwa kupata kura 5,997.
Mpinzani wake mkuu, Robert Kanyinke Ole Kudate wa United Democratic Alliance (UDA), alipata 4,479, akishindwa katika eneo ambalo awali lilikuwa likiunga mkono chama tawala.
Ushindi huu unatafsiriwa kama hatua muhimu kwa Gachagua, ambaye amekuwa akijaribu kujijenga upya kisiasa baada ya kutimuliwa UDA.
Ingawa ODM imeibuka na ushindi katika ngome zake, maswali yanazidi kuibuka kuhusu kama chama kitadumisha umoja au kitapasuka ndani bila Raila.
Kwa upande mwingine, ushindi wa DCP unaonyesha huenda Gachagua akapata umaarufu hasa ikizingatiwa chama chake kilishinda kiti nje ya ngome yake ya Mlima Kenya.