Jamvi La Siasa

Suluhu aingia klabu ya marais wanaoteua jamaa zao serikalini

Na CHARLES WASONGA November 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS Samia Suluhu Hassan sasa anaonekana kufuata mifano ya wenzake wa Uganda, Rwanda na Sudan Kusini na wengine, kuteua watu wa familia yake kushikilia nyadhifa za juu katika serikali yake.

Kulingana na wadadisi hatua hiyo huchochewa na uchu wa marais kutaka kudhibiti asasi muhimu za serikali kwa ajili ya kuendeleza utawala wa kiimla na unaolinda masilahi yao ya kibinafsi.

Alipotangaza baraza jipya la mawaziri 27 na manaibu 29 wa mawaziri, Rais Samia alimteua bintiye Wanu Hafidh Ameir kuwa Naibu Waziri wa Elimu.

Aidha, alimteua mumewe Wanu, Mohamed Mchengerwa, kuwa Waziri mpya wa Afya, katika mabadiliko ambapo mawaziri saba, waliohudumu katika baraza lililopita, walipoteza nafasi zao.

Bi Wanu, ni Mbunge wa Makunduchi katika kisiwa cha Zanzibar ilhali mumewe ni Mbunge wa Rufiji katika eneo la Pwani, kisiwani humo.

Isitoshe, Rais Samia alimteua mwana wa kiume wa Rais wa zamani Jakaya Kikwete, Ridhwani Kikwete, pia aliteuliwa kuwa Waziri wa kusimamia Utumishi wa Umma na Utawala katika Afisi ya Rais.

Mawaziri hao na manaibu wao walioteuliuwa majuma matatu baada ya Samia kutangazwa mshindi katika uchaguzi wa urais uliofanyika Oktoba 29, waliapishwa mnamo Jumanne wiki hii.

Kulingana na Macharia Munene kwa kuteua watu wa familia yake na jamaa za wandani wake, kuwa mawaziri, Rais Samia anafuata mtindo “mbaya” ambao umekuwa ukishuhudiwa Afrika na unaoutumiwa kupanda mbegu za utawala wa kidikteta.

“Sawa na baadhi ya marais wengine katika ukanda huu na Afrika kwa ujumla, inaonekana kuwa Rais Samia anapania kudhubiti asasi kadhaa muhimu serikalini baadhi ya uhalali wa  ushindi wake kuibua  utata. Kando na vyeo vya uwaziri, atateua jamii zake na wandani wake katika nyadhifa zingine kuu serikali ili kuidhibiti wake wa asasi hizo,” anaeleza Profesa Munene, ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amerika (USIU), bewa la Kenya.

Katika nchi jirani ya Uganda, Rais Yoweri Museveni ametua watu kadhaa wa familia yaka kushikilia nyadhifa kubwa serikalini.

Kwa mfano, Mkewe, Janet Museveni ni Waziri wa Elimu na mwanawe wa kiume General Muhoozi Kainerugaba ni Mkuu wa Majeshi nchini humo.

Isitoshe, binti ya Rais Museveni Natasha anahudumu katika Ikulu kama Katibu.

Naye Odrek Rwabogo, ambaye ni mumewe Patience Museveni (binti mwingine wa Rais Museveni) anahudumu kama mmoja wa washauri wa rais sawa na kakake rais huyo Jenerala Caleb Akandwanaho.

Nchini Rwanda, Rais Paul Kagame mwaka jana alimteua bintiye Ange Ingabire Kagame, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Mikakati na Sera katika Afisi yake.

Rais Kagame alitetea uteuzi huo akishikilia kuwa watoto wake pia wako na haki ya ‘kushikilia nyadhifa serikalini’ huku akipuuzilia uvumi kwamba anamwandaa binti huyo kuwa mrithi wake.

Aidha, wana wa kiume wa Rais huyo, Brian Kagame na Ian Kagame, wanahudumu katika Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF).

Nchini Sudan Kusini, mnamo Agosti mwaka huu Rais Salva Kiir mwaka jana alimteua bintiye Adut Kiir kuwa Mjumbe Maalum wa Rais kuhusu Mipango Maalum.

Na katika taifa la Equatorial Guinea, kakake Rais Teodoro Obiang Nguema, Teodoro Nguema Obing Mangue, amekuwa akihudumu kama Makamu wa Rais wa nchi hiyo tangu mwaka wa 2016.

Kulingana na Naibu wa Machakos Francis Mwangangi mwenendo wa marais kuteua watu wa familia zao kushikilia nyadhifa kuu katika serikali zao ni mojawapo ya sifa za  udikteta.