Kimataifa

Tumaini la mapigano ya Ukraine na Urusi kusitishwa laonekana

Na WINNIE ONYANDO, MASHIRIKA November 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer amesema mazungumzo ya kusitisha mapigano nchini Ukraine yanaendelea vizuri.

Akihutubia mkutano wa wajumbe wanaohusika na mazungumzo hayo ya amani kutokea Chumba cha Baraza la Mawaziri katika ofisi zake zilizoko Mtaa wa Downing, Starmer alipongeza na kuikaribisha hatua kubwa iliyopigwa kwenye mazungumzo hayo ya Geneva.

Alisema mazungumzo hayo yalikuwa ni fursa ya kuhakikisha kwamba rasimu ya mpango huo inaakisi kikamilifu maslahi ya Ukraine na inaweka msingi wa amani ya kudumu.

Aliongeza kuwa Ukraine imependekeza mabadiliko kadhaa ambayo yaliungwa mkono na washauri wa usalama wa taifa barani Ulaya.

Wakati uo huo, Rais Donald Trump alisema kwamba mpango wake wa kudhibiti vita nchini Ukraine ‘umerekebishwa’ na atamtuma mjumbe wake Steve Witkoff kukutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin na Waziri wa Majeshi Dan Driscoll kukutana na maafisa wa Ukraine.

Kando na hayo alipendekeza kuwa katika siku za usoni huenda atakutana na Putin na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, ingawa alitahadharisha kwamba hatafanya hivyo kama hakutakuwa na hatua zilizofikiwa kwenye mazungumzo hayo.

Akaongeza kuwa yeye, Makamu wake JD Vance, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth na Mkuu wa utumishi watakuwa wakiarifiwa kuhus mazungumzo hayo kwenye Ikulu ya White House Susie Wiles.

Kupitia mtandao wake wa Truth Social, Trump alisema, bado kuna mambo machache yaliyosalia ambayo bado yanashughulikiwa.

Mjumbe wa rais wa Amerika Witkoff atakutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Moscow wiki ijayo na huenda akaandamana na mkwewe Donald Trump na Jared Kushner, hii ikiwa ni kulingana na rais Trump alipozungumza na waandishi wa habari akiwa kwenye ndege yake ya Air Force One Novemba 25, 2025.