Michezo

Wambui alakiwa na madereva wenzake wa teksi baada ya kutwaa dhahabu Olimpiki za Viziwi

Na GEOFFREY ANENE November 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

DEREVA wa teksi walikaribisha mmoja wao wakati mshikilizi mpya wa rekodi ya dunia na Olimpiki za Viziwi (Deaflympics) ya mita 5,000, Ian Wambui Kahinga, alirejea nchini hapo Ijumaa, Novemba 28, 2025.

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 24 kutoka Nyahururu, Kaunti ya Laikipia, alipokewa kwa shangwe kubwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.

Aliweka historia kwenye makala ya 25 ya Deaflympics yaliyofanyika Tokyo, Japan mnamo Novemba 15-26, baada ya kuvunja rekodi ya dunia na ile ya Deaflympics katika mbio za 5,000m alizoshinda kwa dakika 13:52.83.

Wambui, ambaye hufanya kazi kama dereva wa teksi, alifuta rekodi ya awali ya 14:02.90 iliyowekwa na Mkenya mwenzake Symon Cherono Kibai kwenye Deaflympics za Sofia mwaka 2013.

Wambui alianza mashindano hayo kwa kunyakua dhahabu ya 10,000m katika siku ya kwanza na ushindi wake wa 5,000m ulithibitisha hadhi yake kama mmoja wa wanariadha bora wa walemavu wa kusikia nchini.

Katika JKIA, wapiga ngoma wa kitamaduni, maafisa wa serikali, mkewe Serah Wachira, na msafara mkubwa wa madereva wenzake wa teksi walimkaribisha kwa mbwembwe. “Najisikia vizuri kwa sababu nilipata medali Tokyo na familia yangu iko hapa kunipokea. Nimefurahi sana kuwaona wakitabasamu,” Wambui akasema.

Kwa mafanikio yake hayo makubwa, Wambui atapokea tuzo ya serikali ya Sh11 milioni (Sh3m kwa kila dhahabu na Sh5m kwa kupata rekodi ya duniani) na alisafirishwa kurudi nyumbani kutoka Japan katika sehemu ya heshima.

Wambui aliahidi kuendelea kujituma mazoezini, akisema anatumai mafanikio yake yatachochea wanariadha chipukizi Nyahururu kujituma. “Ninaamini medali hizi zitawatia moyo watu wengi. Wameona kuwa nimevunja rekodi ya dunia, kwa hivyo tukifanya mazoezi pamoja, watahamasika kushinda medali, kuvunja rekodi na kukuwa,” akaongeza.

Mkewe Serah alimsifu kwa bidii na ustahimilivu wake. “Nimefurahi sana na namshukuru Mungu kwa kumsaidia kushinda. Amekuwa akifanya mazoezi kwa bidii, na nitaendelea kumtia moyo ili azidi kupata medali zaidi,” akasema.

Kocha Samuel Kibet alisifu nidhamu na mustakabali mwema wa Wambui, akisema lengo lao lilikuwa kuvunja rekodi za dunia za 10,000m na 5,000m.

“Huu ni msukumo mkubwa kwa wanariadha wote, si walemavu wa kusikia tu. Namshukuru Mungu tulipata mbinu sahihi kwenye 5,000m. Namhimiza aendelee kujituma kwa sababu akipata nafasi zaidi, ataweza kufanya vizuri zaidi,” akasema Kibet. Aliwahimiza wadhamini kuwasaidia wanariadha wenye ulemavu wa kusikia, akisisitiza kuwa msaada zaidi utaibua vipaji vya juu zaidi.