Habari

Familia ya Odinga yamulikwa kwa kuvunja tamaduni kuzika Beryl bomani

Na RUSHDIE OUDIA December 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UAMUZI wa familia ya Odinga ya kumzika Beryl Odinga, dada yake aliyekuwa Waziri Mkuu hayati Raila Odinga, katika boma la baba yao Kang’o ka Jaramogi, umeibua mjadala mkali.

Uamuzi huo sasa umefufua tena mazungumzo kuhusu nafasi ya tamaduni wakati wa maombolezo.

Beryl atazikwa siku Desemba 6, 2025, katika makaburi ya familia ya Odinga Bondo, karibu na kaburi la mamake, marehemu Mama Mary Juma Odinga.

Kwa wengi, familia imechagua umoja na heshima ya kumzika nyumbani.

Lakini kwa wengine, hasa wale wanaoshikilia tamaduni za jamii ya Luo, uamuzi huu unaonekana kinyume na desturi ambazo familia ya Odinga imekuwa ikionekana kama mlinzi wake.

Beryl aliolewa na mume wake wa kwanza, Otieno Ambala, mwaka 1974. Ambala, aliyehusika katika siasa za wakati huo, alifariki kutokana na mshtuko wa moyo mwaka 1985 katika Gereza la Kodiaga. Katika kitabu cha Raila Odinga, The Flame of Freedom, anaeleza jinsi alivyomnusuru dada yake kutoka ndoa ya mateso na kumsaidia kupata makazi Zimbabwe. Beryl alitalikiana na Ambala kabla ya kifo chake, na wakati wa kifo chake alikuwa mjane wa John Tamisayi Mungwari.

Kwa mujibu wa baadhi ya wazee, Beryl alipaswa kuzikwa katika boma la mume aliyewahi kumuoa—iwe Zimbabwe au Gem, Kaunti ya Siaya.

Wiki iliyopita, Raila Odinga Junior alitoa taarifa rasmi ya eneo na tarehe ya mazishi baada ya kikao cha familia kilichohudhuriwa na wajane wa Jaramogi, Betty Oginga na Susan Oginga, pamoja na ndugu wa kambo wa Beryl, Omondi Odinga.

“Kwa baraka za mjomba wangu Dkt Oburu Oginga, tuliketi na Jokawuor na kuchagua sehemu ya mwisho ya kupumzika ya shangazi yangu, Beryl Lillian Achieng Mungwari Odinga, katika Kang’o ka Jaramogi,” alisema Raila Junior.

Baada ya tangazo hilo, mijadala iliwaka katika mitandao na vijijini, wengi wakitilia shaka ishara na athari za kumzika katika boma la baba yake.

Anyango Jabalo, alilalamika kuwa wazee wa jamii wanaruhusu tamaduni kuvunjwa. “Beryl hawezi kuzikwa kama msichana mdogo ambaye hakuwahi kuolewa. Akazikwe Gem au Zimbabwe,” alisema.

Kwa mujibu wake, angefaa kuzikwa kwa Ambala, mume wake wa kwanza.

Aidha, alikosoa wazo la Raila kuzikwa Kang’o ka Jaramogi akisema kuwa tayari ana boma lake Opoda Farm. Alionya kuwa kukiuka desturi huleta mkosi.

Katika desturi za Luo, eneo la mazishi huamuliwa kwa kuzingatia jinsia na hali ya ndoa. Wanaume huzikwa upande wa kulia wa boma na wanawake kushoto. Wanafunzi au mabinti ambao hawajaolewa mara nyingi huzikwa nje ya ua wa boma.

Hata hivyo, familia ya Odinga imepuuza desturi hizo.

Emily Oginga, dada mdogo wa Beryl, alisema maamuzi haya hufanywa baada ya mashauriano ya kina, na si haki kutumia utamaduni kusawiri vibaya marehemu au familia.

Lakini kwa Jotham Ajiki, katibu wa Baraza la Wazee wa Waluo, mazishi ni jambo la kifamilia, na wosia wa marehemu huchukua nafasi ya kwanza.

Mzee Onyango Radier, rafiki wa familia ya Odinga, alisema desturi zinapaswa kuzingatiwa lakini zisichukuliwe kama utumwa. Anaeleza kuwa katika jadi ya Luo, hapakuwa na talaka bali kutengana, na wanawake walizikwa kwa boma la waume wao wa kwanza. Lakini sheria za sasa zinazotambua talaka hufanya hilo lisitekelezeke.