Kilichofanya upinzani kubwagwa chaguzi ndogo
WIKI chache kabla ya uchaguzi mdogo wa Novemba 27, nyota za ushindi zilionekana kumulika mgombeaji wa Chama cha Democratic Action Party ya Kenya (DAP-K) katika eneo bunge la Malava, Bw Seth Panyako.
Vilevile, sauti za kupinga Kenya Kwanza zilipata umaarufu katika Mbeere Kaskazini, jambo ambalo liliunda dhana kwamba kiti hicho kilikuwa tayari cha mgombeaji wa Democratic Party, Bw Newton Karish.
Lakini mnamo Novemba 27, wagombeaji hao wawili walishindwa kwa karibu na wagombeji wa chama cha Rais William Ruto cha United Democratic Alliance (UDA).
David Ndakwa wa UDA alipata kura 21,264, akimshinda Bw Panyako aliyepata kura 19,306, tofauti ya kura 1,958 katika uchaguzi mdogo wenye ushindani mkali. Katika Mbeere Kaskazini, Bw Leonard Muthende alipata kura 15,802, akimshinda Bw Karish aliyepata kura 15,308.
Upinzani umedai vitisho na matumizi mabaya ya rasilmali za serikali.
Siasa za Mbeere Kaskazini ni mchezo mgumu unaokanganya wengi na mara chache unaakisi hali ya kitaifa au umaarufu wa vyama vya siasa. Uhusiano wa ukoo una jukumu kubwa pamoja na mvuto na ushawishi wa mtu binafsi.
Ushindi wa Bw Muthende haukuwa wa karibu zaidi katika jimbo hilo. Mbunge wa kwanza, Sylvester Mate, alimshinda Kamwithi Munyi mnamo 1983 kwa tofauti ya kura 183. Alidumisha kiti hicho katika uchaguzi maarufu wa mlolongo 1988.
Hata hivyo, mwaka wa 1992 alimaliza nafasi ya tano huku tofauti kati ya mshindi (Gideon Ireri Ndwiga) na mpinzani wa karibu zaidi ikiwa kura 486.
Bw Ndwiga alikuwa mbunge pekee aliyechaguliwa kwa tiketi ya Kenya National Congress licha ya eneo kuunga Democratic Party.
Huko Malava, ukosefu wa fedha za kutosha zilizokusanywa kwa kipindi kifupi, vitisho na unyanyasaji wa viongozi wa upinzani pamoja na kupuuza kwa wapiga kura, vilikuwa visiki vya Bw Panyako kupata ushindi.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2022, Bw Panyako alipata kura 20,133 alipokuwa akigombea kwa tiketi ya UDA, lakini alipoteza kwa Malulu Injendi wa Amani National Congress, aliyepata kura 22,981.
Kwa maoni ya Naibu Kiongozi wa Chama cha DCP, Bw Cleophas Malala, uchaguzi huo mdogo uliathiriwa na hongo, vurugu na kutishwa kwa viongozi wa upinzani, na hivyo haukuwa huru, wa haki wala wa kuaminika.