Habari

Gachagua atikisa upinzani kwa matamshi

Na MWANGI MUIRURI December 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MVUTANO umeongezeka ndani ya Muungano wa Upinzani kufuatia kauli za aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwamba chama chake, Democracy for Citizens Party (DCP), kitakuwa chama pekee cha upinzani kuwania viti kaunti ya Nairobi katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Kauli hii imeibua sintofahamu na maoni mseto ndani ya upinzani.

Gachagua alidai chama chake, Democracy for Citizens Party (DCP), kimefikia makubaliano na chama cha Wiper Patriotic Front kuwa chama pekee cha upinzani kuwania viti Nairobi mwaka 2027.

Kauli hii imeibua sintofahamu kubwa ndani ya upinzani na kugawanya maoni ya viongozi na wafuasi.

Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Wiper Patriotic Front, amekanusha kuwepo kwa makubaliano hayo, akisema chama chake hakikubaliani na mpango wowote wa kuipa DCP haki ya kuwania viti vya Nairobi peke yake.

Kauli za Gachagua zimeonekana kama mbinu ya kujitangaza na kuzua mgawanyiko, huku akitambulisha DCP kama “chama kikuu” cha upinzani.

Haya yanajiri baada ya mashambulizi yake makali dhidi ya chama cha Jubilee, ambacho amekiita “Wilibaro Nyekundu” akikifananisha na chama tawala cha UDA, chenye alama ya wilibaro ya rangi ya njano.

Gachagua pia amekosoa vyama vyote vya kisiasa vyenye mizizi eneo la Mt Kenya, akivitaja kama “vikapu vya Rais Ruto kugawanya kura za eneo hilo.”

Aidha, amemtaja Rais Uhuru Kenyatta kuwa “ kiongozi wa zamani na mstaafu” huku akijitambulisha kuwa “msemaji wa sasa na kesho wa Mlima Kenya.”

Vilevile, amedai baadhi ya wenzake katika upinzani wamekuwa “wakiendesha kampeni za mitandaoni bila msingi wa kweli” na kudai kuwa chama cha Jubilee kinaenda kinyume na maadili ya upinzani.

Vinara wengine wa Muungano wa Upinzani ni Martha Karua wa People’s Liberation Party, Eugene Wamalwa wa DAP-Kenya, George Natembeya, Gavana wa Trans Nzoia na naibu kiongozi wa DAP-Kenya, pamoja na Justin Muturi wa Democratic Party.

Jana, Gachagua alisisitiza kuwa hakukosea kuhusu suala la mchakato wa kuteua wagombeaji wa viti Nairobi.

“Nasisitiza kuwa DCP itachukua viti vya Nairobi. Wale wanaopingana nasi wanapaswa tu kueleza nia yao kisha tukutane kwa mashindano,” alieleza.

Aidha, alijitetea dhidi ya lawama za kuendeleza maslahi ya kikabila, akisema: “Ninafanya tu kile kilicho halisi. Ninauza chama changu, kuunganisha na kulinda jamii yangu ili ibaki muhimu katika mjadala wa 2027. Siasa si harusi au ibada ya kanisa,” alisema.

Lakini wanasiasa wengine wametoa tahadhari.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kikuyu, Wachira Kiago, alisema: “Mdomo unaweza kupeleka shingo kwenye kibao cha kifo, mtu asiye na siri ni hatari hata kwake mwenyewe.”

Huku hali ikiendelea kuwa tete ndani ya Muungano wa Upinzani, Gachagua anasisitiza uko imara.

“Tuko washirika imara sana. Hicho ndicho kilichosababisha Kalonzo kuongoza kampeni za DCP Magarini. Ikiwa Ruto anataka kumchukua Kalonzo, lazima aje kuzungumza na Gachagua,” alisema Gachagua.

DCP imesema tayari imeweka mikakati thabiti itakayowezesha vyama vinavyoshirikiana nayo kushinda viti vingi zaidi si Nairobi tu bali kote nchini.

“Tutakaa chini tuseme ni wapi DCP iko imara na inahitaji msaada wa Wiper, Wiper watatupa msaada. Ni wapi Wiper iko imara na inahitaji msaada wa DCP, DCP itasaidia. Huo ndio mpangilio. DCP haipangi kuongoza Wiper, sisi ni washirika,” alisema.

Aliyekuwa waziri wa Kilimo, Bw Mithika Linturi alisema kuwa migongano hii ni ya kawaida wakati wa kuunda muungano, kwani kila kiongozi anajaribu kulinda maslahi yake.