Karibu walimu 60,000 zaidi kuhudumia wanafunzi wanaoingia Gredi ya 10
WANAFUNZI watakaojiunga na Gredi 10 mwezi ujao watahitaji kufundishwa na walimu 58,590 zaidi kwa masomo spesheli chini ya Mtaala wa Umilisi na Utendaji (CBC).
Masomo yaliyoathirika zaidi ni Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu maarufu kama STEM japo mengine pia yameathirika kwa wastani.
Hii ni kwa sababu wanafunzi 569,000, ambayo ni idadi ya juu zaidi, ndio walichagua masomo hayo yenye upungufu wa walimu 35,111.
Masomo ya sayansi ya kijamii yanahitaji walimu 14,630 kisha yale ya sanaa na michezo yana upungufu wa walimu 8,778.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tume ya Kuwaajiri Walimu Nchini (TSC) anayesimamia ubora wa elimu Dkt Reuben Nthamburi, upungufu umepanda kutokana na mfumo mpya wa elimu.
“STEM itakuwa na asilimia 60 ya wanafunzi ambao ni 677,144 kwenye madarasa 15,046. Tulifanya hesabu kwa kutumia darasa ambalo lina wanafunzi 45 ambako tunawahitaji walimu 35,111. Kwa sayansi ya kijamii tunawahitaji walimu 14,630 kisha sanaa na michezo inahitaji 8,778 ambapo idadi ya jumla ni 58,519,” akasema Dkt Nthamburi.
TSC pia ilitoa wito kwa vyuo vikuu na vyuo vya ualimu kuhakikisha mafunzo yao yanaoana na hitaji jipya la soko hasa kwenye masomo ya sanaa na michezo.
Dkt Nthamburi alisisitiza kuwa idadi ya walimu inastahili kuoana na wanafunzi hasa kwenye masomo ya STEM ambayo yamechukuliwa na wanafunzi 569,000 kati ya wanafunzi milioni 1.1 katika Gredi ya Nne.
Wanafunzi hao wanahitaji walimu 35,111.
Masomo ya sayansi nayo yalichaguliwa na wanafunzi 437,000 ambao watahitaji walimu 14,630 nao wanafunzi 124,000 wa Sanaa na Michezo wanahitaji wanafunzi 8,778.
Afisa huyo wa TSC aliwaomba manaibu chansela wa vyuo vikuu na wakufunzi kwenye vyuo vya mafunzo wamakinikie vitengo muhimu katika kuwanoa walimu.