Waangalizi wasema chaguzi ndogo hazikuwa na uwazi
KUNDI la Waangalizi wa Uchaguzi (ELOG) limetoa ripoti ambayo inasema chaguzi ndogo za Novemba 27 zilizingirwa na ghasia, wizi wa kura, kuingiliwa kisiasa na pia mwongozo wa uchaguzi kukosa kuzingatiwa.
Kwenye tathmini yake, ELOG hata hivyo ilisifu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC), kwa kuendesha uchaguzi huo vizuri kwenye mizani ya mipangilio na kiufundi.
Hata hivyo, ELOG ilishutumu IEBC na serikali kwa kukosa kuzuia masuala ambayo yalitia doa uwazi kwenye chaguzi hizo ndogo.
“IEBC ilionyesha uwezo wake wa kiufundi vizuri lakini ikafeli mtihani wa uwazi kwa sababu kura iliingiliwa hata kabla ya raia kushiriki uchaguzi wenyewe,” akasema Mwenyekiti wa ELOG, Bw Victor Nyongesa.
“Uchaguzi wenye uwazi unahitaji vigezo vyote kuzingatiwa na ushirikiano kutoka kwa washikadau wote,” akaongeza.
ELOG ilitaja makabiliano kati ya makundi pinzani katika maeneobunge ya Kasipul, Malava, Mbeere Kaskazini, Nairobi na Machakos wakati wa kampeni.
Kwenye wadi ya Kariobangi Kaskazini, waangalizi hao, walisema walihangaishwa wakati ambapo gari lao lilizuiliwa na wahuni ambao walitaka pesa.
Kundi hilo lilishutumu maafisa wa usalama kwa kukosa kuingilia kati kusuluhisha hali.
“Ni ukiukaji huu wa sheria ambao ulifanya baadhi ya wapigakura kukosa kufika vituoni. Kinachoshangaza zaidi ni kwamba maafisa wa usalama hawakuchukua hatua zozote kuhakikisha kuna usalama na kulinda kura,” akasema.
Waangalizi hao pia walinukuu visa vya utoaji hongo kupitia raia kupewa bidhaa, blanketi na bidhaa nyingine. Kutolewa kwa hongo hizi kwa njia wazi kulizua masuali iwapo chaguzi zenyewe zilikuwa za haki.
Ripoti hiyo ya Elog pia ilitaja watumishi wa umma na maafisa wa kaunti kuingilia kampeni ikiwemo kuzinduliwa kwa miradi ya serikali Baringo siku chache kabla ya uchaguzi huo.
“Watumishi wa umma na maafisa wa serikali kuingilia kampeni kulisaidia upande moja. Sheria inahitaji kuwe na usawa katika uchaguzi,” akasema Bw Nyongesa.
Nusu ya habari feki ambazo zilinakiliwa na ELOG zililenga vyama vya kisiasa na wawaniaji.
Ziliangazia kura za uongo za maoni na pia taarifa za habari ambazo zilijaa propaganda.
Habari zaidi feki zililenga IEBC moja kwa moja ikiwemo habari feki kuhusu usajili wa wapigakura na kubadilishwa kwa vituo vya upigaji kura.
ELOG ilitambua kura feki za maoni, stakabadhi ambazo zilighushiwa na picha ambazo zilibadilishwa.
Licha ya wagombeaji 181 kujisajili kwenye maeneo 22 ambako uchaguzi ulikuwa ukiendelea, ELOG ilisema idadi ya wanawake na vijana ambao walikuwa wakishiriki ilikuwa chini mno.
Katika vituo vya upigaji kura, kulikuwa na ukiukaji mkubwa wa sheria. Katika asilimia 15.2 za vituo vya upigaji kura, wapigakura walichukua picha za karatasi za upigaji kura.
Ilishangaza kuwa kwenye baadhi ya vituo asilimia 90 ya waliojitokeza walisaidiwa kupiga kura.
ELOG pia ilisema kulikuwa na makachero kutoka Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) ambao walivalia nguo za kiraia ndani ya vituo vya upigaji kura.