Habari

Ruku afichua juhudi za kuokoa Gachagua zilivyofeli

Na MWANGI MUIRURI December 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Utumishi wa Umma, Bw Geoffrey Ruku, amefichua jinsi yeye na Naibu Rais, Profesa Kithure Kindiki, walijaribu kumsaidia aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, kuepuka mashtaka ya kumwondoa mamlakani.

Aidha, alitangaza kuwa atapinga vikali juhudi zozote za kuunganisha kura za Mlima Kenya nyuma ya Bw Gachagua kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.

“Tulikaa naye chini mara tatu. Tulijaribu kumfunza jinsi angeweza kunusurika kama Naibu Rais. Tulimwambia awe mnyenyekevu, mtulivu, mwenye heshima na mvumilivu. Hakusikia,” alisema Bw Ruku.

Bw Gachagua tayari amekiri kwamba Prof Kindiki alijaribu kusuluhisha mzozo wake na Rais uliosababisha kuondolewa kwake mamlakani. Alisema hayo katika mahojiano ya moja kwa moja ya Novemba 22, 2025 na vituo vya redio vya lugha ya Embu.

“Prof Kindiki alijaribu kuingilia kati mgogoro wangu na Rais. Aliniambia niwe mvumilivu na mtiifu, niwe mnyenyekevu na niunge mkono rais. Nikakataa. Nilimwambia haiwezekani niwe sehemu ya utekaji watu na mauaji nje ya sheria,” alidai Bw Gachagua.

Kwa upande wake, Waziri Ruku alisema ushauri huo ulipuuzwa, na hivyo Bw Gachagua akachagua kukabiliana na matokeo ambayo yaliishia kumuondoa mamlakani.

Aliongeza kuwa, “Badala ya kusikiliza hekima, Bw Gachagua aliruhusu kiburi, ubabe na dharau vitawale katika miaka yake miwili afisini, na hatimaye akalazimika kutimuliwa.”

Hata hivyo, Bw Gachagua alisema hajutii kuondolewa kwake, akidai amekuwa msaada mkubwa kwa Wakenya, ambao sasa wanamtazama kama mtu pekee anayeweza kuthubutu kumkabili Rais Ruto na kumwambia ukweli bila woga.

Alisema ana “azma tatu zilizosalia: kuunganisha Mlima Kenya, kukuza viongozi chipukizi, na kumuondoa Ruto mamlakani 2027.”

Lakini Bw Ruku alisema Bw Gachagua hataruhusiwa kuelekeza siasa za ukanda huo.

“Mradi Gachagua yuko kwenye picha, Mlima Kenya lazima ugawanyike. Ni heri tugawanyike ikiwa hilo litahakikisha tunabaki serikalini,” alisema.

Alisisitiza kuwa kaunti za Meru, Embu, Tharaka Nithi na sehemu za Kirinyaga lazima ziungane kuhakikisha zinampa Rais Ruto angalau kura milioni mbili mwaka 2027.

Akizungumza katika kipindi cha Kimuri cha Inooro TV, Bw Ruku alisema: “Gachagua lazima aonyeshwe jinsi hana uzito katika eneo hili; ndiyo maana tutazidi kumchukulia kama janga la kisiasa.”

Ili kuonyesha hilo, alisema wanafikiria kumshawishi Rais Ruto kuhakikisha uchaguzi mdogo mwingine katika ngome ambazo Bw Gachagua anajivunia, akidai “tutamshinda.”

Waziri huyo alitangaza pia kuwa kuanzia Mwaka Mpya, Rais Ruto ataanza ziara kubwa eneo la Mt Kenya kuzindua miradi ya maendeleo.

Alisema Rais ananuia kuimarisha uungwaji mkono katika ukanda huo kupitia maendeleo na ushirikiano wa kisiasa, ili kuzuia eneo hilo kuwa nyuma ya Bw Gachagua.

“Hii ni serikali yetu. Mlima Kenya una uwakilishi mkubwa zaidi serikalini mawaziri, makatibu wakuu na nyadhifa nyingine. Sisi ndio tumepokea mgao mkubwa wa maendeleo. Haiwezekani mtu aseme Rais Ruto ni adui wetu,” alisema Bw Ruku.

Aliongeza: “Rais anatupenda kweli. Jambo baya zaidi tunaloweza kufanya ni kuelekeza watu wetu katika upinzani.”

Bw Ruku aliwaonya wapiga kura wa Mlima Kenya dhidi ya kumfuata Bw Gachagua, akisema matokeo ya uchaguzi mdogo wa Mbeere North yanaonyesha hana nguvu yoyote kisiasa.