Lugha, Fasihi na Elimu

NDIVYO SIVYO: Neno chimbua katu si kinyume cha chimba!

Na ENOCK NYARIKI December 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KAMUSI ya Karne ya 21 inaelezea maana ya chimba kama hali ya kufukua ardhi. Nayo maana ya ‘kuchimbua’ ni kufukua ardhi na kufukua udongo.

Tabaini: Fasili nilizozitaja hapa ni zile tu zinazohusiana na mjadala huu. Zipo maana nyingine za kimuktadha ambazo si lengo langu kuzitaja.

Kamusi ya Visawe (1998) ya Mohamed A. na Mohamed S. inatoa visawe vya chimba na chimbua kama ‘zikua’, ‘fukua’ na ‘omoa’ miongoni mwa vingine.

Visawe hivyo vinaelekea kutubainishia kuwa maneno hayo ni mamoja wala hamna unyume miongoni mwayo.

Fasiri ya Kiingereza ya neno ‘chimba’, kulingana na Kamusi ya Kiswahili-Kiingereza (Swahili-English Dictionary) 2001, ni ‘excavate’ au ‘dig’.

Fasiri hizo mbili ndizo pia zinazojitokeza katika neno ‘chimbua’.

Neno ‘excavate’ aghalabu hutumiwa pale ambapo uchimbaji unalenga kina fulani kwa mfano kile cha shimo, tundu, kisima, kaburi n.k. Neno ‘dig’ nalo aghalabu hutumiwa pale ambapo uchimbaji au uchimbuaji si lazima ulenge ukina huo.

Waama, inawezekana kulifukia shimo, kaburi, tundu lililochimbwa au kuchimbuliwa.

Hata hivyo, pale ambapo kitenzi hicho kinahusishwa na chenziwe ‘lima’, sina hakika kuwa shamba lililolimwa linaweza ‘kulimuliwa’!

Kwa njia nyingine, haiyumkiniki kulirejesha shamba lililochimbwa katika hali yake ya kwanza.

Kwa hivyo, kwa mtazamo wangu, huenda isihalisi kudai kuwa kinyume cha chimba ni ‘fukia’ kwani hali hiyo inaegemea fasili moja ya neno hilo; ile ya ‘excavate’.

Kwa muhtasari, neno ‘chimbua’ si kinyume cha ‘chimba’ inavyojitokeza katika vitabu kadha vya sarufi ila kisawe chake.

Hata hivyo, tunapotaka kuelezea ufukuaji wa kitu fulani kilichofichwa udongoni (kilichochimbiwa), neno ‘chimbua’ linaweza kutumiwa kuonyesha unyume.

Yaani, ‘chimbua’ linaweza kutumiwa kama kinyume cha ‘chimbia’ katika muktadha finyu.