Habari

Ripoti yafichua kinachohujumu mpango wa Nyumba Kumi

Na STEVE OTIENO December 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UFISADI miongoni mwa maafisa polisi walaghai, ukosefu mkubwa wa kuaminiana kati ya wananchi na maafisa wa usalama, uwepo wa magenge ya uhalifu na  kujivuta kwa polisi katika kukabiliana na matukio ya uhalifu vinaendelea kuwa baadhi ya vikwazo sugu vinavyozuia ufanisi wa ushirikishaji wa wananchi katika masuala ya usalama nchini.

Miaka kumi na miwili tangu uzinduzi rasmi wa mpango huo chini ya mfumo wa Nyumba Kumi mwaka 2013, Wakenya bado wanakabiliwa na changamoto za kiusalama ambazo ushiriki wa jamii ulitarajiwa kusaidia kupunguza.

Utafiti wa kitaifa uliofanywa hivi majuzi na Kituo cha Kitaifa cha Utafiti wa Uhalifu (NCRC) uliopewa jina Athari za Ushirikishaji Jamii katika Usalama Nchini Kenya”, unathibitisha kwamba licha ya uwekezaji wa miaka mingi, mfumo huo haujafikia kiwango cha usalama na ushirikiano kilichokusudiwa.

Ripoti hiyo, iliyotokana na utafiti kote nchini na mahojiano na wadau muhimu pamoja na majadiliano ya vikundi, ilitokana na utafiti katika kaunti mbalimbali ili kukusanya takwimu na uzoefu halisi wa wananchi.

Ilihusisha wakazi wa kawaida, maafisa wa polisi na viongozi wa utawala wa eneo katika kutathmini kiwango cha ushiriki wa jamii, uelewa wa umma kuhusu mpango huo, mienendo ya uhalifu na kiwango cha kuaminiana.

Mpango wa Nyumba Kumi uliundwa kubadili polisi kutoka kutumia nguvu hadi ushirikiano. Hata hivyo, ripoti inaonyesha malalamishi sugu dhidi ya polisi yakiwemo vitisho, kukamata kiholela, kushirikiana na wahalifu, kupokea hongo na kuchelewa kuchukua hatua unaporipotiwa uhalifu.

Mambo haya yameendeleza ukosefu wa  imani ya umma na kudhoofisha nia ya wananchi kuripoti uhalifu au kutoa taarifa muhimu. Wengi bado wanaogopa kwamba kutoa taarifa kunawaweka hatarini kulipiziwa kisasi na magenge, hasa katika maeneo ambako maafisa polisi wachache wanaaminika kulinda wahalifu.

Changamoto moja kuu ni kuchanganya Nyumba Kumi na mfumo mpana wa kulinda jamii.
“Baadhi ya waliohojiwa walihisi mpango haukueleweka vizuri na hivyo ukachanganywa na Nyumba Kumi,” sehemu ya ripoti inasema.

Katika maeneo mengi, wananchi bado wanachukulia Nyumba Kumi kama muundo tofauti unaoendeshwa na maafisa wa utawala badala ya kuutambua kuwa sehemu ya utaratibu rasmi wa usalama. Kutokuwepo kwa ufafanuzi kumedhoofisha uratibu kati ya polisi, maafisa wa utawala na jamii.

Hata polisi wanakiri kuwa mafanikio hutegemea uongozi wa eneo husika, huku ripoti ikisema utekelezaji umeachwa mikononi mwa makamanda wa vituo, na hivyo kiwango cha utekelezaji hutofautiana kutoka kituo kimoja hadi kingine.

Kutokuwepo kwa mwongozo wa kitaifa kunadhoofisha malengo ya nchi nzima, hivyo baadhi ya maeneo yana ushirikiano mzuri huku mengine yakiwa bila mpango wowote madhubuti.

Pia, utata kuhusu mpango huo umezuia ushiriki. Katika jamii nyingi, baadhi ya watu wanadhani ni kazi ya kulipwa.

“Wengine waliingia wakitarajia kulipwa na wakaacha baada ya kugundua ni kazi ya kujitolea. Hofu ya kuitwa mpelelezi pia inazuia ushiriki katika maeneo yenye magenge,” ripoti inaeleza.

Ingawa asilimia 57 waliripoti kujihisi salama katika maeneo yao, asilimia 43 bado wanahisi kutokuwa salama kutokana na magenge, kesi ambazo hazijatatuliwa, polisi kutochukua hatua haraka, ufisadi na mitaa isiyo na mwanga wa kutosha. Mtazamo huu huathiri mienendo ya watu, kwa mfano, kama watatoka usiku, kuripoti uhalifu au kuwaamini polisi.

Ripoti ilibaini kuwa katika maeneo kadhaa, uhalifu unachochewa na pombe haramu, mtandao wa dawa za kulevya na magenge yanayolindwa na polisi wafisadi.

Pale polisi wanaposhindwa kuchukua hatua, wananchi huchukua hatua zisizo rasmi au hunyamaza.