ZIARA ya Rais William Ruto nchini Amerika wiki hii imegeuka kuwa hatua ya kihistoria katika diplomasia ya kiuchumi, usalama na ushawishi wa kimataifa.

Kwa kusaini makubaliano ya moja kwa moja na utawala wa Rais Donald Trump, ambapo Kenya ndiyo nchi ya kwanza duniani kuingia kwenye mfumo mpya wa ufadhili wa serikali kwa serikali na Amerika, Ruto amedhihirisha uwezo wake wa kuusoma upepo wa kisiasa wa Washington na kugeuza fursa hiyo kuwa maslahi kwa taifa la Kenya.

Kwa mtazamo wa mchambuzi wa mahusiano ya kimataifa, Carol Mutoka, huu si ushirikiano wa kawaida.

Ni ishara kwamba Kenya imetoka kwenye tapo la kupokea misaada na kuingia kwenye daraja la washirika wanaoaminika wa Amerika, wanaoweza kupewa fedha nyingi bila kupitia mashirika mengine.

Katika makubaliano ya kwanza kabisa ya aina yake, Amerika imeahidi kutoa $1.6 bilioni (Sh208 bilioni) moja kwa moja kwa taasisi za serikali katika sekta ya afya badala ya kupitia kwa mashirika yasiyo ya kiserikali.

Hii ni hatua inayotafsiriwa kuwa jaribio la Amerika kuepuka kile Waziri wa Masuala ya Kigeni Marco Rubio aliita kufadhili mitandao ya mashirika yasiyo ya kiserikali “wakati nchi mshirika kama Kenya inakosa usemi kuhusu matumizi ya fedha hizo.”

Rubio aliweka wazi falsafa mpya ya ufadhili wa Amerika kwa kusema “ukitaka kusaidia nchi, fanya kazi na nchi hiyo, si kupitia washirika wanaoiwekea masharti.”

Kwa upande wake, Rais Ruto alisisitiza kuwa makubaliano haya yanaongeza kasi ya mpango wa serikali wa afya kwa wote: “Mfumo huu utaimarisha vifaa vya hospitali, usambazaji wa bidhaa za afya kwa wakati, kuongeza wataalamu na kuleta bima kwa kila Mkenya. Hakuna atakayeachwa nyuma,” alisema Ruto.

Mchambuzi wa sera za afya, Profesa Themba Nyondo, anataja hatua hii kama “kubadilika kwa lugha ya ufadhili kimataifa”, akisema kwamba Amerika inajaribu mfumo mpya unaojenga uwezo wa serikali badala ya kuidhoofisha kwa masharti ya mashirika kama mawakala.

Mazungumzo kati ya Rais Ruto na Mwakilishi wa Biashara wa Amerika, Balozi Jamieson Greer, yamefungua njia ya muundo mpya wa ushirikiano wa kibiashara, hasa baada ya kukoma kwa AGOA mnamo Septemba 2025.

AGOA ilifanikisha mauzo ya zaidi ya mabilioni kwa mwaka na ajira zaidi ya 300,000, hasa katika sekta ya nguo.

Bila mpango mbadala, taifa lingeingia kwenye msukosuko wa ajira na uwekezaji.

Lakini kwa mujibu wa taarifa ya Ruto, makubaliano mapya yamejikita katika sekta za nguo na mavazi, mazao ya kilimo, dawa na kemikali, bidhaa za ngozi, ICT na huduma za kidijitali.

Balozi Greer amependekeza kuongeza AGOA kwa mwaka mmoja, hatua ambayo mchambuzi wa masuala ya uchumi, Dkt Rose Mbiyu, anaiita “kinga muhimu ya mpito inayolinda zaidi ya ajira 100,000 zinazoning’inia hewani.”

Kwa mtazamo wa mchambuzi huyu, Ruto ameisukuma Amerika kuona Kenya si tu kama mnufaika, bali kama mshirika wa kiuchumi mwenye uwezo wa kutengeneza mazingira thabiti ya uwekezaji wa muda mrefu.

Anasema kulingana na kauli ya Waziri Rubio, hatua ya Rais Ruto kupelekea polisi wa Kenya kupigana na magenge nchini Haiti ilichangia pakubwa kushawishi utawala wa Trump kukita na kuendelea ushirikiano wa Amerika na Kenya.

“Ikiwa tungekuwa na mataifa matano au kumi yaliyojitolea kufanya nusu ya yale Kenya imefanya (Haiti), ingekuwa mafanikio makubwa,” alisema Rubio.

Kenya ndiyo nchi ya kwanza kutuma polisi kuongoza operesheni ya kukabiliana na magenge nchini Haiti, jukumu ambalo limeifanya Amerika iitambue kama mshirika anayehitajika sana.

Ruto kwa ujasiri na ukakamavu wake alisisitiza jukumu la Kenya katika kutuliza hali Haiti na kuongeza itaendelea kusaidia.

“Kenya itaendelea kuwa Haiti na kuunga mkono kikosi cha kukabiliana na magenge. Tunashukuru Amerika kwa kututia nguvu,” alisema.

Mchambuzi wa usalama wa kimataifa, Patrick Odhiambo, anaeleza kuwa Amerika kutoa heshima ya kiwango hiki kwa taifa la Afrika ni ishara kwamba Kenya imekuwa mhimili mpya wa usalama wa kimataifa.

“Kwa kutumia lugha isiyo rasmi ya nyumbani, tunaweza kusema Rais Ruto ameingiza Trump boksi kwa kuwa si rahisi kwa kiongozi huyo wa Amerika kuchangamkia nchi ya Afrika hasa wakati huu ambao anaendelea kukazia mataifa mengi yakiwemo jirani ya Kenya,” asema Odhiambo.

Anasema makubaliano kuhusu afya, biashara, na usalama yanaonyesha mkakati mkubwa wa Rais Ruto wa kuhamisha Kenya kutoka kuwa mpokeaji wa msaada hadi kuwa mshirika wa kimkakati wa Amerika.

“Ruto ameutumia vyema muda kumsoma Trump vizuri, na ameweka Kenya kwenye nafasi ambayo mataifa mengi ya Afrika yameitafuta lakini hayajawahi kufikia.”Kwa mara ya kwanza, Kenya inatambuliwa sio tu kwa mahitaji yake, bali kwa uwezo wake, uthabiti wake, na mchango wake kwa dunia.