• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:50 AM
Balala ajitetea dhidi ya madai ya ufisadi

Balala ajitetea dhidi ya madai ya ufisadi

Na PETER MBURU

WAZIRI wa Utalii Najib Balala Alhamisi alijitetea mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Michezo, Utalii na Utamaduni, kuhusiana na madai ya ufisadi katika wizara yake.

Wizara hiyo inadaiwa kupunja Sh100 milioni katika hafla ya muungano wa Maajenti wa Usafiri kutoka Amerika (ASTA)  iliyoandaliwa Jijini Nairobi 2017.

Waziri huyo pamoja na baadhi ya maafisa katika wizara yake tayari wamehojiwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuhusiana na sakata hiyo, ambapo wizara inalaumiwa kuwa ilitoa tenda ya hafla hiyo ya ASTA kuandaliwa bila mashirika mengine kupewa fursa.

Lakini akiwa mbele ya kamati hiyo, Bw Balala alikosoa wanaodai kuwa hafla hiyo ilihusisha utoaji tenda, akisema ilikuwa hali ya Kenya kupigania kuwa mwenyeji wake na kuwa iliinua utalii nchini.

Alisema ijapokuwa uchunguzi kuhusu sakata ya ASTA umekuwa ukiendelezwa dhidi ya maafisa wa wizara yake kwa miezi sita iliyopita, baada ya jina lake kutajwa baadhi ya watu wameingiza siasa katika suala hilo.

“Maafisa katika wizara wamerekodi habari na tume ya EACC kwani uchunguzi umekuwa ukiendelea kwa miezi sita, lakini punde tu jina la Balala lilipotajwa ndipo suala hili limeingizwa siasa,” akasema waziri huyo.

Alisema serikali ilishirikiana na ASTA kuandaa hafla hiyo, serikali ikiwa mfadhili na mwenyeji, nao muungano huo kuwa mwenye hafla haswa.

“Suala la kusema kuwa lilikuwa zoezi la kupeana tenda na kuwa Balala alitafuta kampuni moja ni uongo. ASTA kwanza si kampuni na hakukuwa na zoezi lolote la kupeana tenda. Ikiwa kuna ufisadi ama uvunjaji wa sheria, si Balala,” akasema Bw Balala.

Aidha, alikanusha madai kuwa maafisa wa EACC walivamia nyumbani kwake na afisi yake kuhusiana na sakata hiyo, akitaja habari hizo kuwa feki.

Waziri huyo aidha alizidi kueleza kamati hiyo inayoongozwa na mbunge wa Machakos Mjini Victor Munyaka kuwa kumekuwa na tofauti baina ya wizara yake na zile za Uchukuzi na Miundomsingi, na Michezo na Utamaduni kuhusiana na baadhi ya miradi ambayo zinazozania.

Baadhi ya miradi aliyotaja kuwa na utata ni ujenzi wa barabara kadha ndani ya mbuga ambazo alisema zimekwama kwa kuwa wahandisi wanaoendeleza miradi hiyo wanafanya kazi na wizara ya uchukuzi badala ya ile ya utalii.

Aidha, alitaja usimamizi wa mradi wa Ushanga ambao serikali tayari imetumia mamilioni ya pesa kuupa umaarufu na ujenzi wa makavazi katika shirika la reli Jijini Nairobi kuwa miradi mingine ambayo inafaa kupokezwa wizara ya Michezo na Utamaduni.

You can share this post!

Allegri aapa kuikung’uta Altetico ikizuru Turin

Mswada kielelezo watua bungeni wabakaji wakatwe uume

adminleo