Suluhu akaa ngumu presha ikiongezeka
TANZANIA inaendelea kujikuta katikati ya dhoruba ya kisiasa na kidiplomasia, huku mataifa na taasisi za kimataifa zikitoa matamshi makali dhidi ya hatua zilizochukuliwa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan tangu ghasia za baada ya uchaguzi wa Oktoba 2025.
Kadiri siku zinavyosonga, nchi hiyo inazidi kutengwa, huku msimamo mkali wa serikali ukionekana kufanya hali kuwa mbaya zaidi.
Baada ya uchaguzi ambao viongozi wakuu wa upinzani hawakuruhusiwa kushiriki, maandamano makubwa yalizuka katika miji kadhaa, yakageuka kuwa miongoni mwa ghasia mbaya zaidi nchini humo tangu ilipopata uhuru.
Katika majuma yaliyofuata, habari za vifo, kukamatwa ovyo, na madai ya makaburi ya pamoja ziliibuka na kuifanya Tanzania kuangaziwa kwa namna isiyokuwa ya kawaida duniani.
Serikali, kwa upande wake, imekuwa ikitetea hatua zake.
Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza mara kadhaa kuwa maafisa wa usalama walichukua hatua “za lazima” kukabili kile alichokitaja kama jaribio la “kupindua amani ya taifa.”
Akizungumza wakati wa mkutano jijini Dodoma, Rais Suluhu aliuliza “Mtu akiingia kwenye kituo cha polisi au kuvamia biashara binafsi, anataka nini? Hiyo si haki ya kupinga. Hiyo ni fujo.”
Aliongeza kwamba Tanzania ilikuwa na “kila sababu ya kujilinda” ikizingatia ghasia zilizoshuhudiwa katika baadhi ya mataifa jirani.
Hata hivyo, kauli hizo hazijazima moto wa lawama kutoka nje.
Umoja wa Mataifa kupitia Ofisi ya Kamishna wa Haki za Binadamu ulieleza “wasiwasi mkubwa” kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu, ukitaka mamlaka kuheshimu haki ya kukusanyika kwa amani.
Kauli yao ilionya kuwa kuzima maandamano kwa nguvu hakutaondoa kichocheo cha mgogoro, bali kutaifanya ichipuke tena kwa nguvu zaidi.
Amerika pia haikusita. Kupitia taarifa ya Wizara ya Masuala ya Kigeni, ilisema kuwa inafanyia “mabadiliko makali” uhusiano wake na Tanzania kutokana na kile ilichotaja kama kupungua kwa uhuru wa kujieleza, uhuru wa dini, na mazingira yasiyotabirika ya uwekezaji.
Msemaji wa wizara hiyo alinukuliwa akisema: “Tunafuatilia kwa karibu hatua za serikali ya Tanzania dhidi ya raia wake. Mambo tuliyoyaona hayalingani na misingi ya kidemokrasia tunayopigia debe.”
Ukosoaji
Mnamo Desemba 5, 2025, mawaziri wa Masuala ya Nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola (CMAG) walionya kuhusu hali ya kisiasa na haki za binadamu nchini Tanzania.
Katika taarifa, mawaziri hao walisema kuwa wamehuzunika kutokana na ukiukaji wa misingi ya Jumuiya ya Madola, ikiwemo heshima kwa haki za binadamu, uhuru wa maoni, demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora.
“Taasisi thabiti za kidemokrasia, heshima kwa haki za binadamu, na utawala wa sheria ni muhimu kwa maendeleo endelevu, amani, na usalama,” CMAG iliongeza.
Siku hiyo pia, utawala wa Rais Donald Trump ulitoa onyo jipya kwa wasafiri wanaokusudia kuenda Tanzania, ukiwaonya kutoenda nchini humo kwa sasa kutokana na ripoti za maandamano yanayotarajiwa.
Serikali ya Amerika ilisema imepokea taarifa zinazopendekeza maandamano yanayopangwa kufanyika Desemba 9, 2025, lakini ikawaonya kuwa ghasia zinaweza kuanza mapema mwishoni mwa wiki hii.Mashirika ya kimataifa nayo hayajanyamaza.
The New Humanitarian iliripoti miito ya kufanyika kwa uchunguzi huru wa kimataifa kuhusu vifo vya raia vinavyodaiwa kufikia maelfu.
Vyama vya haki za binadamu vilisisitiza kuwa taarifa za kufutwa kwa nyaraka muhimu na kuzuiwa kwa waandishi wa habari zinaibua wasiwasi mkubwa kuhusu kile wanachokiita “jaribio la kufuta athari za matukio.”
Katika mazingira haya ya sintofahamu, lilizuka suala jipya ambalo limeibua utata zaidi: mwito wa maandamano makubwa ya kitaifa yanayopangwa kufanyika Desemba 9, siku ya Uhuru.
Polisi walitangaza kwa ukali kwamba maandamano hayo ni haramu. Msemaji wa polisi, David Misime, alisema hawakupokea ombi lolote rasmi la maandamano, hivyo yeyote atakayejitokeza atachukuliwa kama “mhalifu anayehusika na kuvuruga amani.”
Aliongeza kwamba waandalizi wa maandamano “walikuwa katika harakati za kugeuza sikukuu ya taifa kuwa uwanja wa vurugu.”
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, sherehe za siku ya uhuru zilifutwa na serikali, ikidai fedha zilizopaswa kutumika kwenye maandalizi zitaelekezwa kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa katika ghasia za uchaguzi.
Wataalamu wa diplomasia wanatafsiri hatua hiyo kama mkakati wa kupunguza joto la kisiasa, huku wakiichukulia pia kama ishara ya wasiwasi mkubwa ndani ya serikali.
Lakini hatua hizi zimeifanya Tanzania ionekane kuwa inazidi kujifungia badala ya kutafuta mazungumzo.
Wanaharakati wa haki za kiraia wanaendelea kukosoa msimamo mkali wa serikali.
Baadhi yao wanasema kukataa kwa serikali kusikiliza madai ya umma na kukimbilia kutumia nguvu ni dalili ya taifa linalopoteza imani ya raia.
Kwa upande mwingine, serikali inatetea msimamo wake ikisema haina budi kuhakikisha “usalama wa taifa.”
Wachanganuzi wa siasa za Afrika wanasema kuwa Tanzania inapitia mtihani unaoweza kubadili kabisa taswira yake kimataifa.
Kila hatua inayochukuliwa sasa—iwe ni kuzima maandamano, kukaza ukandamizaji, au kulaumu ushawishi wa nje, ina athari zake katika mustakabali wa nchi.
“Kinachoonekana wazi ni kuwa Tanzania inatafuta njia ya kujilinda kwa kushikilia msimamo mkali, lakini dunia iko tayari kuiwajibisha kwa matendo yake,” asema mchanganuzi wa siasa na utawala Dkt Isaac Gichuki.