Gachagua amekoroga hesabu za ugavana Kaunti ya Nairobi
WANASIASA wenye azma ya kuwania ugavana Nairobi katika uchaguzi mkuu ujao watalazimika kuanzisha mikakati mipya kufanikisha ndoto zao baada ya madai ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwamba kuna muafaka kwamba chama chake, Democracy for Citizen for Party (DCP) “kiachiwe” kiti hicho; na vile vya useneta na mwakilishi wa kike.
Baadhi ya wale ambao wametangaza nia ya kuwania kumwondoa mamlakani Gavana Johnson Sakaja katika uchaguzi mkuu ujao ni; mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, mbunge wa Makadara George Aladwa, mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya, aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Uchukuzi Irungu Nyakera, mwanaharakati Cyprian Nyamwamu, Waziri wa zamani Moses Kuria, miongoni mwa wengine.
Wachanganuzi sasa wanafasiri kauli ya Gachagua kama inayolenga kukisawiri DCP katika chama ambacho kinavutia, na kitaendelea kuvutia, wafuasi wengi Nairobi baada ya kuandikisha ushindi wa kwanza katika uchaguzi mdogo katika wadi ya Kariobangi North.
“Hii ndiyo maana huku akifahamu fika kwamba ODM ndicho chama chenye ushawishi mkubwa Nairobi, Gachagua alidai kuwa chama hicho sasa kimepoteza umaarufu baada ya kuamua kushirikiana na Rais Ruto katika Serikali Jumuishi. Ndiposa, wiki hii aliwarai viongozi wa ODM kama vile Katibu Mkuu wa Edwin Sifuna na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino kujiunga na DCP,” anasema Herman Manyora.
Kulingana na mchanganuzi huyo, dhana ambayo Gachagua anaendeleza ni kwamba DCP ndicho chama maarufu zaidi Nairobi, ni pigo kwa Bw Owino na wengine ambao wametangaza ndoto ya kuwania ugavana Nairobi katika uchaguzi wa 2027.
“Gavana Sakaja mwenyewe, Mbw Bw Owino, Aladwa na wengine wanaokimezea mate kiti hicho 2027 hawana budi kubadili mikakati kwa kupiga vita dhana inayoendelezwa na Gachagua kwamba wakazi wengi wa Nairobi sasa wanachangamkia chama cha DCP,” anaeleza Bw Manyora.
Akiongea Jumapili wiki jana katika Kanisa la PCEA Kariobangi North, alipohudhuria ibada maalum ya shukrani kutokana na ushindi wa David Wanyoike katika uchaguzi wa udiwani wa Kariobangi North, Gachagua alidai kwamba alikubaliana na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka kuhusu namna ya kugawana viti vya kisiasa Nairobi.
“Tumekubaliana na kiongozi wa Wiper, ambaye amekuwa akisaidia ODM hapa Nairobi. Makubaliano ni kwamba DCP itasimamisha gavana, seneta na mwakilishi wa kike. Pia tumekubaliana kwamba tuchukue viti 16 kati ya 17 vya ubunge na viti 73 vya udiwani kati ya 85,” akaeleza huku akijipiga kifua kwamba DCP sasa ndicho chama chenye ushawishi mkubwa Nairobi kufuatia ushindi wake katika kinyang’anyiro cha udiwani wa Kariobangi North.
Lakini kiongozi Wiper Kalonzo Musyoka amekana uwepo wa makubaliano kama hayo kati yake na Gachagua akishikilia kuwa Wiper itadhamini wagombeaji katika viti vyote vya kisiasa Nairobi.
“Rigathi Gachagua alikuwa akipandisha hadhi ya chama chake cha DCP alipodai kitachukua viti vya ugavana, useneta na mwakilishi wa kike. Japo hamna makubaliano kati yetu na chama cha DCP kuhusu suala hilo, nakubaliana na ujumbe wake kwamba Nairobi sasa imetwaliwa na Umoja wa Upinzani na vyama vya ODM na UDA vitapoteza viti vyote katika uchaguzi mkuu wa 2027,” alifafanua Seneta wa Makueni Dan Maanzo.
Mchanganuzi wa siasa Tom Mboya hata hivyo, anasema kuwa ushindani utakuwa mkali zaidi katika kaunti ya Nairobi na Bw Gachagua asidhani kuwa mgombeaji wa DCP atafaulu kwa urahisi.
“Kwanza, hakuna takwimu zinazoonyesha kuwa chama cha DCP kimepata umaarufu mkubwa Nairobi baada ya kushinda kiti kimoja cha udiwani. Pili, Nairobi ni kaunti yenye wakazi kutoka maeneo na makabila mbalimbali nchini na mwaniaji wa ugavana sharti avutie uungwaji mkono kutoka kwa watu hao wote. Hii haitakuwa kazi rahisi jinsi Gachagua anavyoonekana kudhani,” anaeleza.